Rais wa Sri Lanka Maithripala Sirisena amefanya mabadiliko katika vikosi vya usalama nchini humo.
Sirisena amefanya uamuzi huo baada ya maafisa kushindwa kuchukua hatua licha ya kupokea taarifa za uwezekano wa kutokea mashambulizi yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 350 wakati wa kipindi cha Pasaka.
Katika hotuba ya televisheni kwa taifa, Rais Sirisena alisema atambadilisha mkuu wa vikosi vya majeshi katika kipindi cha masaa 24, na Jumatano aliwataka katibu wa ulinzi na mkuu wa jeshi la polisi kujiuzulu.
Bado hakutaja nani atakayechukua nafasi zao. Sirisena amesema alifichwa taarifa hizo za uwezekano wa kutokea mashambulizi na ameahidi kuchukua hatua kali dhidi ya maafisa wote walioshindwa kumuarifu mapema.