Munir Shemweta-KILOSA
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema wizara itapitia upya mashamba yote yaliyofutwa na Rais katika Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.
Lukuvi alikuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Chanzulu, Wilaya ya Kilosa alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi katika wilaya hiyo ikiwa ni jitihada za wizara kumaliza migogoro ya ardhi nchini.
Alisema katika maeneo mbalimbali yapo mashamba yaliyofutwa na Rais lakini hayajawekewa utaratibu wa kuyatumia na hivyo kutoa fursa kwa wajanja wachache kujigawiwa na mengine kuyauza kwa wananchi bila kufuata utaratibu.
Alisema katika kuhakikisha mashamba yote yaliyofutwa na Rais katika Wilaya ya Kilosa na kuzua mgogoro baina ya wananchi na wamiliki, wizara imeamua kupeleka timu kutoka wizarani kwa ajili ya kuyafanyia uhakiki mashamba yote yaliyofutwa katika wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa Lukuvi, timu hiyo inajumuisha Kamishna wa Ardhii, Mary Makondo, Kaimu Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Samweli Katambi, Mthamini Mkuu wa Serikali Evalyne Mugasha, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kati Ezekiel Kitlya na wataalamu kutoka Idara za Mipango Miji wizarani.
Alisema uamuzi wa kwenda na timu kutoka wizarani unalenga kumaliza migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo hasa baada ya kubaini ofisi za wilaya na Mkoa wa Morogoro kushindwa kutatua mgogoro huku viongozi wa wake wakituhumiwa.
Waziri alitaja kazi kubwa itakayofanya timu hiyo kuwa ni kupitia mashamba 15 yaliyofutwa na rais na kufufua mipaka ya mashamba hayo na kazi hiyo itafanywa kwa na ushirikiano wa ngazi za wilaya.
“Tutayapitia mashamba yote yaliyofutwa na rais na kujua kilichomo ndani yake na timu ya uhakiki niliyokuja nayo itanilitea mapendekezo ya namna ya kutumia mashamba na mengine watapewa wanaostahili na si kila mtu atapewa,” alisema Lukuvi
Huku akishangiliwa na wananchi wa Chadulu, Lukuvi alisema wale wote waliojimilikisha mashamba yaliyofutwa na Rais watanyang’anywa na kupatiwa wanaostahili na mengine yatatolewa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa ajili ya kupatiwa wawekezaji.