Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
SERIKALI imesema itaendelea kuondoa urasimu na kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa taasisi binafsi na za umma ili kuleta maendeleo nchini.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, wakati akizindua nembo mpya ya Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), itakayoitambulisha na kuonyesha historia ya ukuaji wake tangu ianzishwe mwaka 1996.
Bashungwa alisema kuwa anaridhishwa na mchango wa SBL katika kukuza uchumi wa nchi hivyo, anaahidi kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara kwa ajili ya kampuni pamoja na biashara.
“Maboresho yanayaofanywa kwa sasa kwenye sera yanalenga kuondoa urasimu usio wa lazima kwa taasisi za umma ambao ni kikwazo kwa maendeleo na ukuaji wa biashara,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Mark Ocitti, alisema kuwa nembo hiyo mpya inawakilisha ubora, ubunifu, utaalamu, urafiki na kujiamini.
“Nembo hii pia inaonyesha kuwa kampuni yetu inatengeneza bia zake kwa viungo asilia, pia ni kielelezo cha historia pamoja na vipindi ilivyopitia kampuni kwa miaka yote tangu ikimiliki kiwanda kimoja kidogo cha kuzalisha bia jijini Dar es Salaam, hadi kufikia kampuni kubwa inayomiliki viwanda vitatu vilivyopo Dar es Salaam, Moshi na Mwanza, huku ikitoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 800,” alisema Ocitti.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SBL, John Ulanga, alisema nembo hiyo mpya inaakisi lengo jipya la ukuaji wa kampuni hiyo na kuongeza kuwa SBL imewekeza Paundi za Uingereza milioni 14 katika shughuli zake na upanuzi. “Uwekezaji huu mkubwa, utasaidia kutengeneza ajira mpya zaidi, utaongeza mchango wa SBL kwenye kodi serikalini,” alisema.
Mwisho