Benki ya Exim yazindua kampeni ya mkopo wa nyumba

0
1304

BENKI ya Exim Tanzania imezindua kampeni maalum ya miezi mitatu kuhusiana na ofa yake ya mikopo ya nyumba za makazi kwa riba ndogo ikilenga kurahisisha umiliki wa hitaji hilo muhimu kwa wateja wake na watanzania kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mikopo Binafsi, Biashara ndogo na za kati wa benki hiyo,  Charles Kapufi, kampeni ya huduma hiyo inayofahamika kwa jina “Nyumba Yangu Loan’’ inahusisha utoaji wa mikopo mipya ya nyumba yenye riba ya asilimia 15 tu, ikiwa ni kiasi cha chini kutolewa kwa mikopo ya aina hiyo sokoni.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo jijini Dar es Salaam, Kapufi alisema kuwa kupitia huduma hiyo ya Nyumba Yangu Loan, walengwa watanufaika na mikopo sahihi kwa gharama nafuu na rahisi.

“Kununua nyumba ni uamuzi muhimu sana kwa mtu yoyote, iwe mara yako ya kwanza au la! Ingawa mahitaji kati ya wanunuzi hawa yanatofautiana, umuhimu wake ni sawa. Ndio maana kupitia huduma hii mikopo ya ununuzi wa nyumba, kila mteja atapewa mkopo kulingana na hitaji lake na sio kwa kanuni jumuishi,’’ alifafanua.

Alisema huduma hiyo inatoa suluhisho pia kwa wale wamiliki wa nyumba ambao wana mikopo yenye riba kubwa kwenye taasisi mbalimbali za fedha kwa kuweza kubadilishiwa mikopo yenye marejesho makubwa kwenda kwenye marejesho yenye riba nafuu na Benki ya Exim.

“Kana kwamba hiyo haitoshi, kwa wateja ambao nyumba zao zimeongezeka thamani kutokana sababu kadhaa ikiwemo ongezeko la bei au uboreshaji walioufanya kwenye nyumba hizo tumejipanga kuwawezesha kubadilisha ongezeko hilo kuwa pesa kupitia mkopo maalumu ambao wanaweza kuutumia kujenga nyumba nyingine, kuboresha zaidi nyumba au kuwekeza fedha hizo kwenye uwekezaji wa mambo mengine,’’ alisema.

Aliongeza kuwa, ikiwa ni sehemu ya wadau muhimu katika kusukuma gurudumu la maendeleo hapa nchini, benki hiyo imejitoa kuwa mstari wa mbele katika kubuni huduma ambazo zinaleta tija zaidi kwa wateja ikiwemo kuwawezesha wateja wake na watanzania kwa ujumla waweze kumiliki nyumba hizo kwa kuwapatia mikopo yenye mashariti nafuu.

“Ni imani yetu kwamba, hili litafanikiwa kwa kupitia ushauri na namna tunavyojitoa kuwahadumia wateja wetu  kama sehemu ya familia yetu, kwani tunawasaidia katika kila hatua ya mchakato wa maombi ya mkopo, kupitia hatua rahisi. Tunaamini kwamba kumiliki nyumba nzuri kunahitaji huduma nzuri ya kifedha na hiyo ndio maana halisi ya Nyumba Yangu Loan,” alisema

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here