Na Esther Mnyika Mtanzania Digital
Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana Taasisi ya Kimataifa Mifumo ya Chakula (AGRA) na Kampuni ya John Deer zinatarajia kuanza mchakato wa kuwashindanisha vijana kwenye vikundi na kuwapatia zawadi ya trekta lengo likiwa kuendelea kuhamasisha vijana kuingia kwenye kilimo.
Hayo ameyasema leo Septemba 8, jijini Dar es Salaam Waziri Kilimo, Hussein Bashe wakati akikabidhiwa Trekta na Kampuni ya John Deer ambapo amesema mchakato ukianza vijana watapaswa kuandaa andiko la wazo la kilimo wanachotaka kukifanya na kikundi watakachoshinda watakabidhiwa trekta hiyo.
“Tutatangaza mashindano vijana wataleta maandiko watakaoshindana, wazo lao la biashara na namna ya kufanya biashara katika shughuli za uzalishaji mkakati huo wa kupata mshindi utakuwa wa wazi,” amesema Bashe.
Amesema kikundi ambacho kimeshinda watakabidhiwa trekta Ili kuangalia namna vijana watakavyoenda kufanya kazi za kilimo kibiashara.
Amesema Mwelekeo wa serikali ni kujaribu kutafuta mbinu za kiwaingiza vijana katika kilimo, sio kila kijana atakuwa na shamba, kunamwingine atalima, mwingine atauza mbegu mwingine atatoa huduma za gani,” amesema Bashe.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa mbegu bora za mazao ya chakula nchini amesema zinahitajika Sh billion 650 kuhakikisha mbegu hizo zinazalishwa nchini
Bashe amesema Sekta binafsi ilizindua mbegu ya kitanzania mwaka 2021 huku uwezo wetu wa kuzalisha mbegu ndani ya nchi ulikuwa asilimia 20 na mahitaji yetu ya mbegu kwa mwaka huu wa kilimo yalikuwa tani 120,000.
Ameongeza kuwa Watanzania ndani ya nchi wamezalisha tani elfu 60 ambayo sawa na asilimia 50, ya mahitaji na njia iliyoweza kuongeza uzalishaji ni mbili ikiwepo makadirio ya mahitaji na mahitaji halisi.
Amesema makadirio ya mahitaji kwenye kilimo ni makubwa sana lakini mahitaji halisi ni tani 120,000 ya mbegu za mazao yote.
“Tumeweza kufika asilimia 50 ya uzalishaji serikali inaendelea kuwekeza kwenye mashamba ya umma, mwaka jana tumeanza kujenga miundombinu ya umwagiliaji na si muda mrefu tutazindua mashamba ya serikali yaliyowekewa miundombinu ya umwagiliaji ya kisasa ambayo yatatumika kwaajili ya uzalishaji wa mbegu,” ameongeza Bashe,
Amesema katika mashamba 17 ya serikali atakayezalisha katika hayo mashamba sio serikali ni sekta binafsi ya ambazo zitakua zinajihusisha na uzalishaji wa mbegu.
Amesema serikali imeweke nguvu kwenye utafiti ili kuweza kuleta mbinu bora za kilimo cha kisasa, na waweze kuwapa sekta binafsi waweze kuzalisha kwa wingi.
Amesema maelekezo ya rais ndio welekeo serikali ifikapo 2025 asilimia 75 za mbegu bora na mazoa ya chakula zizalishwe nchini na si kuagiza kutoka nje.