NA CLARA MATIMO- MWANZA
SERIKALI imeshauriwa kutatua tatizo la upungufu wa matundu ya vyoo kwa wanafunzi wa shule za msingi nchini, ili kuwaepusha kupata magonjwa ya mlipuko.
Ushauri huo ulitolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji Ubongo na Uti wa Mgongo wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC), Dk. Emmanuel Kanumba, alipozungumza na MTANZANIA kuhusu athari ambazo wanafunzi wanaweza kuzipata kutokana na changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo.
Dk. Kanumba, alisema endapo wanafunzi watakabiliwa na upungufu wa matundu ya vyoo wanaweza kujikuta wakiambukizana mradhi mbalimbali kutokan ana kujisaidia ovyo nje ya majengo ya shule.
Hali hiyo husababisha kuibuka kwa magonjwa yaenezwayo kwa njia ya hewa na kushikana mikono kwa sababu shule nyingi hazina maji.
“Magonjwa ya mlipuko huenea kwa kasi na madhara yake ni makubwa kwa sababu husababisha vifo vingi endapo wagonjwa hawatapata matibabu sahihi kwa wakati.
“Naishauri Serikali ilipe suala la matundu ya vyooo katika shule za msingi kipaumbele kwa sababu wanafunzi wanaosoma shule hizo bado ni watoto.
“watoto wa shule za msingi siku hizo ni wadogo na hawana uwezo wa kujikinga na kujilinda ni mwanafunzi wa darasa la kwanza au la pili akihitaji kujisaidia akienda chooni akamkuta mwenzake hawezi kuvumilia atajisaidia nje ya tundu la choo, kuzuia ni bora kuliko kutibu,”alisema.
Aliiomba Serikali kulipa kipaumbele suala la matundu ya vyoo hasa kwa shule za msingi ili kuepuka kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko kama kipundupindu.