33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Samia aagiza bidhaa za kilimo ziwe na ubora

Na SARAH MOSES -DODOMA


MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka wakulima, wajasiriamali na wadau wa sekta zingine kuhakikisha bidhaa zao zinafikia ubora wa hali ya juu kuanzia shambani zinakozalishwa, zinakosindikwa na kuhifadhiwa hadi kumfikia mlaji.

Akizungumza jijini hapa jana wakati akizindua Tamasha la Mvinyo ambalo ni la kwanza kufanyika katika historia ya maendeleo ya sekta ya zabibu nchini, alisema kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu kutawezesha kuhimili ushindani wa soko ndani na nje ya nchi na kuuzwa kwa bei nzuri.

“Kipekee niwaase wananchi wa Dodoma kuendelea na juhudi za kuongeza uzalishaji na usindikizaji wa zao la zabibu,” alisema na kuongeza kuwa kwa sasa asilimia 70 ya mvinyo unaouzwa nchini unatoka nchi za nje.

“Watanzania tupende vya kwetu maana waswahili husema thamini chako hadi cha mwenzako usikione kama kitu.

“Ni ukoloni mamboleo kutumia bidhaa za nje ambazo mara nyingi hatujui malighafi zake zimezalishwa vipi hadi zinapoingia sokoni na kudharau vya kwetu ambavyo tuna uhakika wa uhalisia wake,” alisema.

Alisema ana mpango wa kufanya ziara jijini hapa kwa kutembelea na kuhamasisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo kilimo cha zabibu.

“Nawataka wakulima, watafiti wasindikaji na wasambazaji na washiriki kubadilika kutoka kilimo cha kujikimu na kufanya kilimo cha biashara kwa kufuata kanuni za kilimo bora zenye kuongeza tija ya mazao,” alisema.

Alizitaka halmashauri zote, mashirika ya umma na binafsi yanayojihusisha na kilimo kwa mikoa ya kanda ya kati wawe na mipango ya kuongeza maeneo ya umwagiliaji hasa katika kipindi ambacho dunia inashuhudia mabadiliko ya tabianchi.

Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema zabibu ni moja ya mazao yanayoweza kuongeza mapato kutoka nje na aliishauri Serikali kuangalia mahali ambako wakulima watakuwa wanauza zao hilo kwa bei nzuri.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda cha kusindika mvinyo cha Dompo, Archard Kato, alisema lengo la tamasha hilo ni kutangaza zabibu za Dodoma ili kuongeza mapato ya ndani.

“Serikali ikiweka mazingira mazuri kwa kushirikiana na wadau kikiwamo Kituo cha Utafiti wa Kilimo watasaidia uzalishaji na kilimo chenye tija,” alisema Kato.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles