27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

SAFISHA SAFISHA NDANI YA CCM: TUMEELEZWA UKWELI?

WAKATI wa mchakato wa kutafuta mgombea wa kiti cha Urais wa kukiwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka 2015, mambo mengi yalitokea ambayo yalionesha kukitikisa chama hicho.

Zaidi ya wanachama 40 walichukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuwa mgombea Urais kwa tiketi ya chama hicho, na ni jina moja lililokuwa likisikika zaidi kati ya wanachama wengine wote, hasa kutokana na wingi wa mashabiki aliokuwa nao.  Mwanachama huyo alikuwa Mheshimiwa Edward Lowassa.

Hata hivyo, ilipotokea kwamba Kamati ya Maadili ilikata jina la Lowassa na majina ya wagombea wengine, huku ikibakiza majina matano tu, taharuki ilitokea.  Wengi wa wanachama walilalamika kwamba utaratibu wa kuchuja wagombea haukufuatwa, huku wengine wakienda mbali zaidi na kutamka hadharani kwamba hawakubaliani na yaliyotokea.

Watu watatu ambao walikuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, ndio waliokuwa na uthubutu wa kuzungumza na wanahabari, wakisema kwamba hawakubaliano na kitendo cha majina ya baadhi ya wagombea “wanaopendwa” kukatwa.

Watatu hao, Sophia Simba, Dk. Emmanuel Nchimbi na Adam Kimbisa walifanya kitu ambacho hakikutarajiwa. Hali haikurudi kuwa shwari, kwani Mkutano Mkuu wa CCM ulipoitishwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama wakati huo, Rais Jakaya Kikwete, kuingia ukumbini, idadi kubwa ya wajumbe walikuwa wakiimba “Tuna imani na Lowassa”. 

Sisi watazamaji tulikuwa tukisubiri kuona kama CCM wameufunika ukurasa ule na kuamua kujenga chama kwa kuunganisha wanachama wote ili watumie nguvu zao katika kuitekeleza ilani ya chama chao, hasa kutokana na wao kuongoza Serikali.  Hata hivyo, kauli iliyotolewa na Rais John Magufuli wakati akikabidhiwa Uenyekiti wa chama hicho mwaka jana, ilidhihirisha kwamba kipo kitu kinakuja.

Siku hiyo, Rais Magufuli alilalamika kwa Rais Kikwete kwamba kulikuwa na watu walioonyesha utovu mkubwa wa nidhamu kwa kuimba wana imani na mtu fulani.  Akaenda mbali zaidi kwa kusema kwamba ingekuwa amri yake, basi siku hiyo angeondoka na karibu nusu ya watu waliokuwa ukumbini.  Miezi kadhaa baadaye, ahadi hiyo ambayo wakati huo hatukutambua kwamba ilikuwa ahadi imetimia.

Wikiendi iliyopita ilisheheni taarifa juu ya safisha safisha iliyofanywa ndani ya CCM.  Taarifa za kufukuzwa kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba na wanachama wengine, kutolewa kwa onyo na kuamriwa kuomba msamaha Dk. Emmanuel Nchimbi na kusamehewa kwa Adam Kimbisa, kumeibua gumzo na maswali mengi.

Katibu Mwenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alieleza kwamba watu hao walikutwa na makosa yaliyotokana na utovu wa nidhamu ulioonyeshwa wakati wa Uchaguzi Mkuu. Hilo ndilo linaloibua maswali mengi: Je, ni kosa kwa wanachama kupingana na jambo ambalo wanaona halikufanyika ipasavyo?  Kwa kutumia uhuru wao wa kuzungumza na kuonyesha msimamo tofauti na wa “wakubwa” huo ni utovu wa nidhamu?

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema kwamba upinzani wa kweli utatoka ndani ya CCM.  Kwa miaka mingine hilo limekuwa likitokea kwa kiasi fulani, lakini kilichotokea katika kuelekea uchaguzi mkuu uliopita, kilidhihirisha kauli hiyo.  Upinzani wa kweli ulitoka ndani ya CCM na sidhani kama hilo ni kosa. 

Upinzani maana yake ni kupingana kwa lengo la kufikia lengo moja kwa njia tofauti na katika kupingana huko, kila mwanachama anakuwa na upande anaoupigia debe, hakuna kosa.  Inapofikia hatua ya watu kuimba kuwa wana imani na fulani, basi hiyo ndiyo demokrasia yenyewe ya watu kusema kile wanachokiamini.  Hakuna sheria iliyovunjwa, wala hakuna utovu wa nidhamu uliofanyika.  Kukubaliana tu na kila kitu hata kama hukiafiki moyoni, ni unafiki.

Bado siamini kwamba wanachama waliofukuzwa, waliosimamishwa, waliopewa onyo na waliosamehewa, wametendwa hayo kutokana tu na kilichotokea wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu.  Sitaki kuamini kwamba kutumia uhuru wako wa kutoa maoni ni hatia ndani ya CCM na sitaki kuamini kwamba safisha shafisha iliyotokea ni kwa sababu tu ya kile kilichotokea kipindi kile.  Nataka kuamini kwamba yapo mengine ya ziada ambayo pengine CCM inachelea kuyasema.  Pamoja na kuchelea kwao kuyasema, nadhani ni haki yetu kuujua ukweli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles