25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

LAITI NINGELIKUWA MAKONDA….

INAKARIBIA mwezi sasa suala la vyeti vya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam linaendelea kuzungumzwa kila kona ya nchi, kwa watoto wa mjini wanasema hivi sasa Bashite ndio habari ya mjini. Naingia kwenye mtandao wa kijamii kuangalia hili na lile nakutana na maneno yasomekayo kama “acha maneno weka vyeti acha kulialia weka vyeti” yakiambatanishwa na alama ya reli ili kuyakoleza na kuweka msisitizo.

Ama kweli Bashite ndio habari ya mjini, maana kila kona habari ni Bashite, lakini ikabidi nijiulize nini hasa kinachofanya mjadala huu uendelee kuwa gumzo kiasi hiki? Hivi mtuhumiwa mwenyewe hili halimkeri? Baada ya kulitafakari vyema nikagundua kuwa anayefanya mjadala huu uwe mrefu ni Makonda mwenyewe na si mtu mwingine yeyote. Kwa nini nasema yeye mwenyewe ndiye sababu? Hebu tuangalie mambo yafuatayo tuone nini kingefanyika kama ningelikuwa Makonda.

Kwanza kabisa isingenihitaji mimi kulia ningekuwa nacheka muda wote, kwa nini kicheko? Kwa sababu ningekuwa na vyeti visivyo na utata wowote, ingetoka wapi sababu ya mimi kulia kanisani, kwa nini nilie wakati nina uhakika kuwa mimi ni Paul Makonda  na si Daudi Bashite kama wasemavyo, yaani nilie wakati nasoma kwa kuwa nilisoma kwa shida halafu walimwengu nao waje kuniliza tena na wakati  pa kusemea nnapo na nina uhakika wa kutosha halafu nitafute sehemu niende kulia wananchi wanionee huruma kwa nini? Ningelikuwa Makonda ningekuwa nacheka tu.

Pili, ningeita vyombo vya habari huku nikiwa nina ushahidi wa kutosha, ningeanza kwa kuwaonesha cheti cha kuzaliwa, cheti cha ubatizo kama kipo, vyeti vyangu vinavyoonesha ngazi tofauti za elimu niliyopitia huku pakiwepo na walimu wangu kama ningefanikiwa kuwapata ili waje watoe ushuhuda kama mimi ndie Paul Makonda au ni Daudi Bashite na wakati wananifundisha nilikuwa natumia jina gani. Natumai baada ya kufanya hili suala ningekuwa nimekata mzizi wa fitina na ndio ungekuwa mwisho wa kuitwa  Daudi Bashite, utata ungetokea wapi kama ningemuita Mwalimu wangu Kawiche aliyenifundisha darasa la tatu pale Shule ya Msingi Minazi Mirefu au Mwalimu Mruma aliyenifundisha darasa la saba pale Shule ya Msingi Bryceson, wa sekondari je, nafikiri nisingebakisha hata wale walionifundisha chuo nao ningewaita waje kuthibitishia ulimwengu kwamba mimi si Daudi Bashite.

Tatu, kama baba na mama yangu  wako hai basi nafikiri wao ndio wangekuwa wasemaji wa mwisho, hata kama niliwahi kubadilisha jina nafikiri wao ndio wangekuwa na sababu za kutosha kwa nini nilibadilisha jina, sidhani kama wazazi wanaweza kuja kuzungumza kwenye vyombo vya habari wakaongopa hata kwenye kipindi kama hichi ambacho vyombo vya habari vinausaka ukweli wa jabo nyeti kama hili kwa gharama yeyote.

Nne, baada ya kufanya hayo yote hapo juu jambo la nne ambalo ningelifanya ni kuwaruhusu wale wote wenye ushahidi juu yangu ya kuwa nimeghushi vyeti vyangu basi waweke ushahidi hadharani na yeyote atakayenituhumu na ikabainika hana ushahidi wa kutosha basi ningemfikisha mbele ya mahakama ili anisafishe jina langu na iwe fundisho kwa wengine.

Haya ni baadhi ya mambo ambayo yangetokea kama ningelikuwa Paul Makonda lakini ikumbukwe tu kuwa haya yangetokea kama sijaghushi vyeti vipi kama ningekuwa nimeghushi je, ningekaa kimya kama alivyo kimya Mheshimiwa? Ama kweli ukitaka kuzijua shuruba za safari vaa viatu vya msafiri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles