Anna Potinus – Dar es salaam
Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz, amesema kuwa anaamini klabu ya Yanga haiihitaji kumilikiwa, kufadhiliwa na mtu binafsi bali inatakiwa kuendeshwa na wanachama wenyewe.
Ametoa kauli hiyo leo Juni 20, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es salaam ambapo amesema kuwa anaamini mfadhili atainyima timu hiyo kuwa na sauti na kufanya maamuzi yao wenyewe.
“Timu kama Yanga haitakiwi kumilikiwa binafsi na haitakiwi kuwa na mfadhili kwasababu ni timu ya mamilioni ya watu na unapokuwa na mtu binafsi anamiliki timu muhimu yenye historia kama hii inawanyima wanachama mamilioni sauti muhimu katika klabu yao,” amesema.
Aidha amewataka watu kuachana na imani ya kuwa mdhamini ndio muarobaini wa Yanga kufanikiwa kwa kuwa klabu nyingi zinazomilikiwa na watu binafsi huwa zinaanguka na kwamba Kuna klabu nyingi duniani ambazo zinaendeshwa na wanachama na zimefanikiwa.
Rostam pia ametoa ufafanuzi juu ya kiasi cha fedha cha shilingi milioni 200 alichokitoa kwenye harambee ya kuichangia klabu ya yanga ‘kubwa kuliko’ iliyofanyika wiki iliyopita na kiasi alichotoa leo katika harambee ya kuichangia timu ya Taifa ya Taifa Stars kiasi cha shilingi milioni 30 ambapo amesema kuwa Taifa Stats inaenda kushiriki mashindano ya muda mfupi lakini Yanga inaendelea na ligi hivyo ina matakwa makubwa zaidi
“Watu wanahoji kwanini nimetoa fedha nyingi kwa Yanga kuliko Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ hii timu imeenda kushiriki mashindano ya AFCON mwaka huu lakini Yanga inaendelea na ligi siku zote hivyo ina matakwa makubwa kuliko Stars,” amesema.