Anna Potinus – Dar es salaam
Mfanyabiashara maarufu nchini Rostam Aziz amevunja ukimya juu ya ushabiki wake kwa klabu ya Yanga ambapo amesema kuwa amekuwa akiishabikia timu hiyo kwa kipindi kirefu na kwamba amekuwa akiisaidia kimya kimya bila kujiweka hadharani.
Ametoa kauli hiyo leo Juni 20, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es salaam ambapo amesema kuwa ameanza kuishabikia timu hiyo tangu yupo darasa la kwanza.
“Katika harambee ya Yanga kuna watu wengine walichomeka vitu vyao kwenye mitandao lakini mimi ni shabiki wa Yanga tangu niko darasa la kwanza mpaka leo lakini nimekuwa shabiki wa Yanga wa kabatini ambae sio wa makelele,” amesema.
“Nimekuwa nikiichangia Yanga kimyakimya sasa nilivyochangia hadharani katika harambee ya juzi watu wakaanza kuzungumza maneno mitandaoni,” amesema.
Aidha amesema kuwa kumekuwa na misukosuko mingi katika uendeshaji wa timu nchini na kwamba wamekuwa wakijaribu mambo mengi ambayo sio endelevu ikiwamo ufadhili na hivyo kuwataka kuachana na suala hilo na kujitahidi kuwa na uongozi bora.
“Yanga sio timu ya kawaida ina historia ndefu sana, imeanzishwa mwaka 1935 na ina wanachama mamilioni na hakuna timu yenye historia ndefu kama hiyo hivyo ni lazima uangalie mfumuo unaotakiwa uwepo katika uendeshaji wake,” amesema.
Aidha Rostam amesema kuwa kuna umuhimu wa vilabu kuweka uwanja sawa kwa kila mdhamini kuweka bidhaa yake kudhamini timu, na kuahidi kuwa iwapo kutakuwa na biashara yoyote atakayoweza kuitumia katika kuidhamini Yanga atafanya hivyo.