30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Rostam amshukia Slaa

Rostam ANa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

ALIYEWAHI kuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, amesema kauli zilizotolewa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa kuwa alimpigia simu za vitisho ni kauli za uongo, ubinafsi na upotoshaji.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Rostam alisema: “Nilimsikiliza Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Willibrod Slaa jana alipokuwa akizungumza katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

“Kwa mara nyingine kama ilivyo hulka yake miaka yote, Dk. Slaa kathibitisha pasi na shaka kwamba yeye ni mtu mwongo, mbinafsi na mpotoshaji mkubwa.

“Nimesikitishwa na kushtushwa japo sikushangazwa hata kidogo na hatua ya kiongozi huyo ambaye sasa anaonekana kukubuhu kwa uzushi kutoa matamshi ya namna hiyo.”

Rostam alisema hajawahi hata mara moja kuwa na mawasiliano na Dk. Slaa wakati wowote, na kwamba madai yake kuwa alimtisha ni ya kupuuzwa na hayana msingi.

Alisema ni jambo lisiloingia akilini kwa watu wanaomfahamu Dk. Slaa kwamba eti yeye anaweza kufika hatua ya kumtishia maisha na akakaa kimya bila kuchukua hatua za kumshtaki  polisi.

“Ili kuthibitisha madai yake hayo, namtaka Dk. Slaa ajitokeze hadharani na kutoa ushahidi wa jambo hilo,” alisema na kuongeza:

“Hakuishia hapo alikwenda mbali na kudai kwamba eti mimi naisaidia Chadema. Huu ni uongo mwingine wa dhahiri. Namtaka Dk. Slaa kutoa ushahidi pia katika madai yake haya.

“Ni huyu huyu Dk. Slaa ambaye mwaka 2010 alizusha kwamba eti mimi, tukiwa na Rais Jakaya Kikwete na Edward Lowassa tulikutana katika Hoteli ya La Kairo Mwanza na kupanga njama za kumwibia kura zake za urais.

“Wakati Dk. Slaa akitoa madai hayo ya uongo, mimi nilithibitisha kwamba wakati huo nilikuwa Afrika Kusini na  Rais Kikwete alikuwa Lindi, huku Lowassa akiwa Arusha. Ni wazi kwamba tusingeweza kukutana La Kairo kama alivyodai yeye.

“Si hilo tu, ni Dk. Slaa huyo huyo ambaye wakati fulani aliwahi  kumzushia Rais Kikwete alipodai kwamba eti rais alilazimika kusafiri hadi China kwa usiku mmoja na kurejea Dar asubuhi kwenda kumtoa mtoto wake aliyedai kwamba alikuwa ametiwa mbaroni huko China.

“Ni Slaa huyu huyu ambaye mwaka 2010 wakati wa kampeni, alifikia hatua ya kuutangazia umma wa Watanzania kwamba kulikuwa na malori yaliyobeba kura za CCM ambazo zingesaidia ushindi wa wizi yaliyokamatwa Tunduma. Malori hayo yalipokaguliwa yalibainika kuwa na mizigo ya kawaida,

mtu wa namna hii  kwa Kiingereza anaitwa ‘pathological liar’.

Kwangu mimi Dk. Slaa anacho kipaji kimoja tu cha uongo na si cha kuwatumikia wananchi kama alivyodai mwenyewe.

“Kwa kifupi Dk. Slaa ni mchanganyiko wa mtu mbinafsi, mbumbumbu na mwongo, mchanganyiko ambao huzaa chuki.

“Kama alivyosema yeye mwenyewe  jana, mtu anayepotosha watu wanyoofu anapaswa kufungwa  jiwe na kutupwa baharini, basi Dk. Slaa ndiye hasa anayepaswa kufungwa jiwe na kutupwa baharini kwa sababu ya usugu alioujenga katika upotoshaji wa mambo, uzushi na uongo uliokubuhu”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles