MADRID, HISPANIA
KLABU ya Real Madrid leo hii inatarajia kushuka dimbani kwenye uwanja wa nyumbani wa Santiago Bernabeu na kuwakaribisha wapinzani wao Barcelona katika fainali ya pili ya Kombe la Supercopa de Espana.
Mwishoni mwa wiki iliyopita fainali ya kwanza ilipigwa kwenye Uwanja wa Camp Nou, huku wenyeji Barcelona wakikubali kichapo cha mabao 3-1, hivyo inaweza kuwa kazi nyepesi kwa Madrid kumalizia mchezo huo wa leo.
Real Madrid watamkosa mshambuliaji wao hatari, Cristiano Ronaldo ambaye anatakiwa kutumikia adhabu ya michezo mitano aliyosimamishwa baada ya kumsukuma mwamuzi kwenye mchezo huo wa wiki iliyopita.
Kwenye mchezo huo Ronaldo alifunga bao moja na kuoneshwa kadi ya njano kwa kuvua jezi wakati akifurahia bao hilo, lakini alioneshwa kadi nyekundu dakika chache baadaye kutokana na kujiangusha kwenye eneo la hatari, baada ya kuoneshwa kadi hiyo aliamua kumsukuma mwamuzi, hivyo kusababisha kufungiwa michezo mitano.
Hata hivyo, kwenye mchezo huo wa leo Madrid wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kutokana na ubora wa kikosi chao msimu huu, wakati huo Barcelona wakihitaji ushindi wa mabao 3-0 ili kutwaa taji hilo.
Kazi kubwa itakuwa kwa Barcelona hasa katika safu ya ushambuliaji ambayo inashuka dimbani kwa mara ya pili bila ya mshambuliaji wao hatari, Naymar aliyejiunga na kikosi cha PSG ya nchini Ufaransa wiki mbili zilizopita.
Kuondoka kwa Neymar kunawafanya washambuliaji, Lionel Messi na Luis Suarez kuwa na kazi kubwa ya kuipita safu ya Real Madrid, hata hivyo safu ya kiungo ya Barcelona inaonekana kupungua kasi.
Hata hivyo, chochote kinaweza kutokea kwenye mchezo huo kwa kuwa soka ni mchezo wa makosa, Barcelona waliwahi kufanya makubwa kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa msimu uliopita dhidi ya PSG hatua ya makundi, huku mchezo wa kwanza Barcelona wakifungwa mabao 4-0 kabla ya marudiano Barcelona wakishinda mabao 6-1 na kuingia hatua ya robo fainali.
Leo hii Barcelona hawana nafasi kubwa ya kuwa mabingwa, lakini wanaweza kushinda. Wachezaji ambao wanaweza kuanza kwenye kikosi cha kwanza ni pamoja na Ter Stegen, Aleix Vidal, Gerard Pique, Samuel Umtiti, Jordi Alba, Ivan Rakitic, Sergio Busquets, Denis Suarez, Lionel Messi, Luis. Suarez na Gerard Deulofeu.
Madrid wanaweza kuanza na Keylor Navas, Dani Carvajal, Sergio Ramos, Raphaël Varane, Marcelo, Luka Modric, Casemiro, Ton Kroos, Gareth Bale, Kareem Benzema na Isco.