26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

MADIWANI CHALINZE WAPATA MAKAMU MWENYEKITI

Na GUSTAPHU HAULE-PWANI

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Mkoa wa Pwani, limemchagua Diwani wa Kata ya Mandela, Madaraka Mbode (CCM), kuwa makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo.

Mbode atakayeshika nafasi hiyo kwa miaka mitatu ijayo, alichaguliwa juzi wakati wa uchaguzi uliofanyika Mjini Lugoba, wilayani hapa.

Pamoja na uchaguzi huo, madiwani hao walipitia pia taarifa za utekelezaji katika kipindi cha mwaka 2016 na mapitio ya mwaka 2017/18.

Mbali na Mbonde, wengine waliochaguliwa ni Diwani wa Kata ya Kiwangwa, Kwaga Malota (CCM) aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti Kamati ya Elimu, Afya na Maji pamoja na Hassan Mwinyikondo ambaye ni Diwani wa Kata ya Msoga (CCM) aliyeshinda nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Said Zikatimu, alisema uchaguzi huo ulifanyika kikanuni na kwamba Mbode alishinda bila kupingwa kwa kupata kura 16 za madiwani wote.

“Kupatikana kwa makamu mwenyekiti huyo pamoja na wenyeviti wa kamati, kutasaidia kuleta msukumo wa kimaendeleo katika Halmashauri ya Chalinze. Kwa hiyo, naomba madiwani tuendeleze ushirikiano ili tupate maendeleo haraka,” alisema Zikatimu.

Kwa upande wake, Mbode aliwashukuru madiwani hao kwa kumuunga mkono, huku akisema yupo tayari kushirikiana nao katika kutatua changamoto za wananchi wa Chalinze.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Edes Lukoa, aliwaomba madiwani hao kuendelea kushirikiana ili kutetea masilahi ya halmashauri yao.

Kwa upande wake, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM), aliwataka madiwani hao kusimamia kikamilifu ilani ya CCM kwa kutekeleza yale yanayohitajika kwa wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles