NA AMON MTEGA-RUVUMA
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme ametoa siku tano kwa halmashauri za wilaya kuhakikisha fedha za miradi ya maji zilizokuwa kwenye akaunti zao kuhamishiwa kwenye akaunti ya za Wakala wa Usambazaji wa Maji Safi na Mazingira Vijijini (Ruwasa) ili mamlaka hiyo iweze kukamilisha miradi kwa wakati.
Agizo hilo alilitoa jana wakati akisimamia makubaliano na kukabidhiana mikataba baina ya halmashauri na RUWASA mjini Songea.
Alisema fedha zinazotakiwa zihamishiwe kwenye akaunti ya wakala huo, ni zaidi ya Sh bilioni moja ambazo zitatumika kakamilisha miradi mikubwa ya maji.
Alisema baadhi ya miradi hiyo, imekuwa ikisuasua kutokana na kutokusimamiwa kikamilifu kwa wakandarasi waliopewa kazi.
Alisema hadi kesho fedha hizo ziwe zimeshahamishwa na siyo vinginevyo na kuwa miradi hiyo itakamilika kwa kutumia mfumo wa fosi akaunti.
Alisema Rais Dk. John Magufuli ameunda chombo hicho ili kufanikisha kusambaza maji kwa wananchi kwa wakati.
Alisema miradi hiyo, itafanyiwa kazi na wakala wenyewe kwa kushirikiana na wananchi hadi ifikapo mwaka 2020 huduma hiyo iwe imewafikia asilimia 85 au zaidi na kufanya kila maeneo ya vijiji na mijini kutokuwa na tatizo la maji.