SAKATA la wanafunzi hewa jijini Mwanza kwa mara ya tatu limechukua sura mpya baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kuunda tume ya tatu iliyohusisha idara ya usalama wa taifa, polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), baada ya kubainika ripoti ya tume mbili zilizopita ina uwalakini.
Hatua hiyo imetokana na tume mbili za awali kuchunguza sakata hilo na kutoa taarifa ambayo imeonyesha baadhi ya walimu wastaafu, marehemu, walioteuliwa na Rais Dk. John Magufuli kuwa wakuu wa wilaya sambamba na wale waliohama shule kwenda nyingine wamehusika katika ongezeko la wanafunzi hewa 5,559.
RC mongella amesema sakata la wanafunzi hewa ni zito na kuwatumia salama watumishi ambao wanajua walidiriki kutoa taarifa za uongo wajiandae kisaikolojia kupoteza nafasi zao na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria huku akibainisha kwamba Mkoa wa Mwanza una wanafunzi hewa 13,000 .
Akizungumza jana jijijini Mwanza wakati akipokea msaada wa vitabu vya aina mbambalimbali vya shule ya sekondari, msingi, vitabu vya kilimo na ufugaji vilivyotolewa na Klabu ya Igoma Rotary, Mongella alisema ameshtushwa na taarifa ya marehemu kuandikiwa barua ya kujieleza juu ya wanafunzi hewa.
RC Mongella alisema anafuatilia kwa ukaribu sana juu ya taarifa iliyowataja walimu wastaafu, waliofariki na wale walioteuliwa ma kuhamishwa lakini wameingizwa katika sakata hilo la wananfunzi hewa ambapo tayari ameunda tume yake na kuipa siku 14 kumpatia taarifa kamili.
“Tunafanya uchambuzi upya wa majina ya walimu waliorodheshwa, nisema wazi atakayehusika ajue hatapona, kwanza kama anajijua aanze kwenda nyumbani kwao,” alisema.
Juzi Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Mwanza, kilimpatia Mkurugenzi wa jiji hilo, siku tatu kuwaomba radhi juu ya taarifa yake aliyoitoa kwenye vyombo vya habari kwa kuwavua madaraka, kuwasimamisha kazi na kuwadhalilisha walimu, vinginevyo watamfikisha mahakamani.