DERICK MILTON-SIMIYU
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, amesema mkoa wake hautawaweka karantini watu ambao wanatoka Dar es salaam, Arusha, Mwanza na Zanzibar baada ya kutangazwa kuwepo wagonjwa wenye virusi vya Corona (COVID-19).
Mtaka alisema amekuwa akipokea ujumbe kutoka kwa wananchi wa mkoa huo na kusoma kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo whatsap, wakitaka watu wanaotoka kwenye mikoa hiyo wawekwe Karantini.
Alisema hayo jana wakati akizindua zoezi la upuliziaji dawa kwenye mabasi yaendayo mikoani katika stendi kuu ya magari hayo Bariadi.
Alisema amepokea ujumbe na kuona watu wengi wakitaka mkoa utangaze uhamuzi huo, jambo ambalo alisema hawezi kulifanya kwani halijatangazwa na viongozi wakuu wa nchi.
Mtaka alibainisha kuwa katika kupambana na ugonjwa wa corona ambao tayari umeingia nchini, ipo kamati ya kitaifa inayolishughulikia ikiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye ndiyo mwenye mamlaka ya kutangaza uhamuzi huo.
“ Nimetumiwa meseji nyingi, nimeona hata kwenye mitandao ya kijamii, wananchi wa mkoa wetu wametaka watu wanaotoka Dar es salaam, Mwanza, Arusha na Zanzibar maeneo ambayo kuna maambukizi ya ugonjwa huu wawekwe karatine,” alisema Mtaka…
“ Nimeona nia yao wakitaka kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu, niwaeleze kuwa kama mkoa hatuwezi kufanya hilo jambo, muhimu kila mtu ajikinge kwa kufuata masharti yote ambayo yanatolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya,” aliongeza Mtaka.
Pia aliziataka ofisi za waganga wakuu wa halmashuari na wakuu wa askari wa usalama barabarani, kuhakikisha wanapulizia dawa magari yote kwenye stendi za Wilaya kila siku.
Aidha aliwasisitiza wananchi wa mkoa huo kuhakikisha wanachukua tahdhari dhidi za kujikinga na ugonjwa huo na kuacha tabia ya kupuuzia wanayoelekezwa na wataalamu.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa, Festo Dugange, alisema hadi sasa watu 120 wamekwa karantini katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, huku 18 wakiwa tayari wameruhusiwa baada ya kutokutwa na dalili za ugonjwa huo na 102 wakiendelea kukaa karantini.
Alisema watu hao walisafiri kutoka nje ya nchi na maeneo mengine ndani ya nchi huku baadhi yao wakijipeleka wenyewe karantini baada ya kujihisi wana dalili zote za ugonjwa huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa, Henry Mwaibambe, alisema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha magari yote yanazingatia sheria ikiwemo kutozidisha abiria ikiwa pamoja na kupuliziwa dawa kila siku.