26.5 C
Dar es Salaam
Friday, September 24, 2021

Hotuba ya tatu ya upinzani yakataliwa bungeni

 RAMADHAN HASSAN -DODOMA 

SPIKA wa Bunge,Job Ndugai amezuia kusomwa hotuba ya kambi rasmi ya upinzani bungeni ya Sheria na Katiba kwa madai kwamba imekiuka kanuni za Bunge. 

Hotuba hiyo ilitakiwa kusomwa na Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo wa Katiba na Sheria,Salome Makamba. 

Kutokana na kukataliwa huko,Mnadhimu wa Kambi hiyo,Ester Bulaya amedai kwamba watapeleka malalamiko katika Ofisi ya Spika wakidai kwamba wanaonewa na hawatendewi haki. 

Hiyo inakuwa hotuba ya tatu ya Kambi rasmi ya upinzani kuzuiliwa kusomwa bungeni ambapo ya kwanza kukataliwa ilikuwa ya Ofisi ya Waziri Mkuu na kisha ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira. 

Jana baada ya Mwenyekiti wa Bajeti,Mashimba Ndaki kumaliza kuwasilisha hotuba ya kamati hiyo alisimama Spika Ndugai na kuzuia hotuba hiyo isisomwe kutokana na kukiuka baadhi ya kanuni za Bunge. 

Spika Ndugai alisema hotuba hiyo inashida na inaoekana imeandikwa na mtu ambaye yupo nje kabisa ya Bunge. 

“Maana ukiisoma hotuba kwanza tuanze nini madhumuni ya kikao hiki waziri wa Sheria na Katiba amewasilisha hotuba kwamba Bunge likubali kupitisha makadirio ya mapato na matumzi ya Wizara ya sheria na Katiba 2020-2021. 

“Hotuba hii ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho haugusi bajeti hakuna hotuba, kama zinaelekea zinaandikwa na mtu fulani mahali ukiangalia hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati iliyosomwa na Najma Giga na mnayo humu tazama na mtaona inavyojielekeza kwenye ‘subject matter’ 

“Tazama hutuba ya Mwenyekiti wa bajeti inavyoielekeza kwenye subject matter hotuba ya upinzani haikatiliwi baadhi ya mengine ambayo mmeyaweka lakini si mjielekeze kwenye swali? 

Spika Ndugai alisema ni kama darasani lazima ujibu kile ambacho umeulizwa ukijibu tofauti utakuwa umekosa yote na umetoka nje ya mstari. 

“Nawaombeni sana sio mara ya kwanza mmeshiriki sana kule kwenye kamati na mavitabu yote mmeyapata yasomeni mjue Waziri anakujaje na nyinyi mje vipi,”alisema. 

Alisema kubwa linalomsumbua ni kuhusiana na kambi hiyo kufanya mashambulizi kwa mhimili mwingine ambao ni mahakama. 

“Lakini kubwa na linalonisumbua zaidi tumesisitiza mara kwa mara kwamba sio mhimili wa Bunge ndio iwe center ya mashambulizi kwa Mahakama. 

“Nimetafakari sana lakini sipendi kuona hamsomi hutuba zenu lakini katika mazingira haya nafanyaje na Salome (Makamba) naye ni mwanasheria,Kiongozi wa upinzani ni mwanasheria na wapo wanasheria wengine wengi, mhimili wa mahakama tuuheshimu kuonesha kabisa mahakama ya Tanzania sio chochote hapana haipendezi hata kidogo. 

“Kwa hiyo kwa sababu ya kuwa nje kabisa ya kinachojadiliwa hotuba hii sitairuhusu isomwe dakika zetu mtaongeza wachangiaji na nitawapa nafasi. 

Bulaya na Malalamiko 

Kwa upande wake,Bulaya alisema watapeleka malalamiko kwa Spika wa Bunge kutokana na kutotendewa haki katika mambo mbalimbali pamoja na Ofisi ya Katibu wa Bunge. 

“Na heshimu maamuzi yako kwa sababu kiti chako ndicho chenye Mamlaka lakini, sio maamuzi yanayotolewa na kiti kama chama tunaridhika nayo na kwa mujibu wa kanuni,tutatumia kanuni ya tano kuleta ‘official’ ofisini kwako. 

“Na Mheshimiwa Spika wakati unatoa maamuzi umesema hatutajielekeza kwenye bajeti,nikuhakikishie hotuba hizo tunaandika wenyewe na tunajua tunachokifanya na nini tunataka kueleza na kuishauri Serikali. 

Bulaya alisema ni wajibu wao kuandika changamoto za Wizara kiujumla na hivyo na ndivyo ambavyo wamekuwa wakifanya kila siku. 

“Lakini na sisi tutakuja kukuona tumekuwa tuna malalamiko yetu hatutendewi haki kama kamati nilipenda nili-adress mbele ya Bunge lako kama ambayo wewe umetoa ‘ruling’ na ninasisitiza tunaiheshimu mbali ya kuiheshimu kuna vitu na sisi tutakuja kukuona ili huko tunakoenda tuende vizuri,”alisema Bulaya. 

Akijibu,Spika Ndugai alisema Ofisi yake itapokea maombi hayo na ana uhakika watapewa haki pamoja na kuelekezwa jinsi ya kuandika hotuba zao. 

“Siku hizi hatufanyi siri hotuba ya waziri ilikuwa haijulikani lakini sasa hivi kila mnacho mmepokea ripoti zote unapokuja hebu angalieni. 

“Tutapokea maombi yenu na kwa hakika mtapewa haki labda itawasaidia wenzetu kupitia na kuona jinsi gani mpo nje ya mstari kabisa na sio nje ya mstari kidogo 

“Na bahati mbaya sana Spika wenu ni mwanasayansi ndio bahati mbaya nyingine tutasaidiana huko,sisi wanasayansi hatupotezi muda nikiulizwa swali elezea kuhusu azimio la Arusha naelezea tu,”alisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
157,854FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles