PENNSYLVANIA, MAREKANI
RAIS wa Marekani Donald Trump ameadhimisha siku 100 madarakani kwa kutoa hotuba inayokejeli wanahabari na kutetea mafanikio yake.
Trump aliwaaambia wafuasi wake jimboni hapa juzi kuwa ameridhika kuwa pamoja nao badala ya wanahabari aliopaswa kuhudhuria nao dhifa ya chakula cha jioni.
Imekuwa utamaduni wa muda mrefu kwa Ikulu ya Marekani, kutumia matukio ikiwamo siku 100 za urais madarakani kuhudhuria hafla hiyo maarufu mjini Washington.
Akihutubia umati, Rais Trump amelinganisha na kutofautisha, kile alichotaja 'siku 100 za wanahabari kushindwa na kazi yao', na mafanikio yake aliyodai yametokana na kutimiza ahadi zake kila siku.
Miongoni mwa ahadi hizo alisema ni pamoja na kurejesha ajira za viwanda na kumaliza mzozo katika sekta ya makaa ya mawe.
Pennsylvania ni jimbo linalotegemea uchumi wa uchimbaji madini, na lilikuwa muhimu katika uchaguzi wa mwaka jana.