Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Kanisa la Uamsho na Matengenezo ya Kiroho, limeandaa kongamano la maombi maalum ya kuliombea Taifa pamoja na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan yatakayofanyika Aprili 28,2024 kwenye viwanja vya Suma JKT, Mwenge jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 23,2024, jijini, Kiongozi wa kanisa hilo, Mwalimu Augustine Tengwa amesema Mungu ndiye aliyemsemesha juu ya maombi hayo kutokana na agano lake kwa Tanzania.
“Tangu mwezi wa kwanza aliponiambia Mungu, sikusema. Mungu amenisemasha mambo ambayo yatabeba ajenda ya siku hiyo ya maombi. Mungu kaniambia vitu vya kumuombea Rais,”ameeleza.
Amesema sababu kubwa ya kuamua kuliombea Taifa na Rais Samia ni kutokana na kuwa kiulimwengu hakuna Taifa ambalo halifanana na Tanzania hasa katika amani.
Mwalimu Tengwa amesema kuna mabadiliko ya kiuongozi ambayo Mungu anayaingilia kati, hivyo kuwataka watu wa dini zote kujitokeza katika maombi hayo.
“Nataka habari hii iende nchi nzima kuwa huu msimu wote ambao Mungu amenisemesha kuanzia huu mwezi wa nne tutakuwa na maombi mfurulizo ya kumuombea Rais na Taifa hadi muda wa uchaguzi ili kuondoa uovu,” amesema.