Na Mwandishi wetu
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan leo Septemba 30, 2024, amezindua Kitabu kuhusu Maisha na Uongozi wa Hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania mwaka 1977 -1980 na 1983- 1984, uzinduzi huo umefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Rais Samia amesema mafanikio ya uongozi wa Hayati Sokoine yalichangiwa na uaminifu kwa mamlaka yake ya uteuzi, mapenzi kwa wananchi, uadilifu na uchapakazi.
Amesema maisha ya kiongozi huyo yalikuwa na mafunzo mengi na kuacha alama katika kila jukumu alilosimamia.
“Hayati Sokoine alitekeleza wajibu wake kikamilifu kama msimamizi wa shughuli za kila siku za Serikali katika kipindi kigumu na kusimama imara katika kipindi ambacho nchi ilikumbwa na changamoto za kiuchumi, uhaba wa chakula, miundombinu duni na changamoto katika sekta za viwanda na afya,”