NAIROBI, KENYA
WABUNGE wa Chama cha Jubilee wamedai kinara wa muungano mkuu wa upinzani wa NASA, Raila Odinga, anashirikiana na mataifa ya kigeni kula njama za kujitangaza mshindi wa uchaguzi wa urais na kwenda kuapishwa nchini Tanzania.
Hayo ni kwa mujibu wa wabunge watatu wa chama hicho na majimbo yao kwenye mabano, Muthomi Njuki (Chuka/lgambangombe), Moses Kuria (Gatundu Kusini ) Kimani Ichungwa (Kikuyu) na Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Tharaka Nithi, Beatrice Nkatha.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara mjini Chuka, Kaunti ya Tharaka Nithi, wabunge hao walisema lengo la Raila kutaka muungano wa NASA kuwa na kituo cha kuhesabu kura ni kujitangaza mshindi kisha aende kuapishwa katika nchi jirani ya Tanzania.
Walionya hatua hiyo itazua ghasia baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8 kama ilivyotokea baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.
Viongozi wa Jubilee wamekuwa wakipinga azma ya NASA kuwa na kituo cha kuhesabu kura wakisema ni Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) pekee inayoruhusiwa kisheria kuhesabu na kutangaza matokeo.
“Tunajua Odinga anapanga kujitangaza mshindi na kwenda kujiapisha Tanzania akishindwa kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 8,” alisema Icungwa.
Alisema kujitangazia matokeo ya uchaguzi mkuu ni sawa na uhaini kwa sababu hilo ni jukumu la IEBC pekee kufanya hivyo.
Njuki alidai ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 zilisababishwa na kukataa matokeo ya uchaguzi mkuu kulikofanywa na Odinga.
Kuria alisema Odinga anahisi kushindwa na hivyo anatafuta njia za kupinga matokeo.