PARIS, UFARANSA
BINGWA namba mbili kwa ubora wa nchini wa tenisi duniani kwa upande wa wanaume, Rafael Nadal, juzi alionesha ubora wake na kutwaa ubingwa wa French Open baada ya kumchapa mpinzani wake Dominic Thiem kwa seti 6-3, 5-7, 6-1, 6-1.
Pambano hilo ambalo lilitumia saa tatu na dakika moja, lilimfanya Nadal kuonesha ubora wake kwa wachezaji wa mchezo huo kwenye udongo.
Kuna viwanja mbalimbali vya viwanja ambavyo vinatumika kwa ajili ya mchezo huo, miongoni mwa viwanja hivyo ni pamoja na sehemu yenye udongo, hivyo Nadal ameripotiwa kuwa bingwa wa viwanja hivyo.
Huu ni ubingwa wake wa 12 wa michuano hiyo ya wazi ya nchini Ufaransa, lakini bado hajamfikia mpinzani wake Roger Federer ambaye anashika nafasi ya tatu kwa ubora, lakini anaongoza kuwa na mataji mengi ya Grand Slam ambapo anayo 20, huku Nadal akiwa na 18.
Hata hivyo, Nadal amempongeza mpinzani wake Thiem kwa ushindani aliouonesha kwenye mchezo huo wa fainali huku akiamini anaweza kuja kufanya makubwa kwenye michuano mingine siku za hivi karibuni.
“Ameonesha ushindani ambao sikuutarajia, amestahili kufika fainali, nampongeza kwa kile alichokifanya, ninaamini atakuja kuwa bora zaidi ya hapo kwa siku za hivi karibuni kama vile kwenye michuano ya Austrian.
“Msimu huu ushindani ulikuwa mkubwa sana, lakini kila mmoja alipambana kuhakikisha anafanya vizuri, ninaamini nimeweza kutwaa ubingwa huu kutokana na maandalizi yangu kuwa bora zaidi.
“Ninawashukuru wote ambao walikuwa na mimi katika kipindi hiki chote tangu mwanzo hadi siku ya mwisho ninatwaa ubingwa, nianze kwa familia yangu, mke wangu pamoja na mashabiki kwa kuonesha sapoti ya nguvu kwangu, ninaamini bila ya wao sidhani kama ningekuwa na nguvu ya kufanya hivi, asanteni sana,” alisema bingwa huyo.