SOCHI, Urusi
RAIS wa Urusi, Vladimir Putin amesema kwamba nchi yake bado inaendelea na msimamo wake wa kuisaidia Uingereza katika kuchunguza tukio la kupewa sumu kachero wake wa zamani, Sergei Skripa
Kwa mujibu wa Shirika la Habari nchini hapa, TASS, Rais Putin aliyasema hayo mwishoni mwa wiki, baada ya kukutana na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel aliyekuwapo ziarani.
Alisema, alivyoahidi tangu mwanzo serikali yake ina dhamira ya dhati kuwa sehemu ya uchunguzi huo na kwamba licha ya kuwa bado hawajajibiwa, lakini wapo tayari kufanya hivyo.
“Narudia kusema tena sisi tunataka kusaidiana na Uingereza katika kuchunguza tukio hilo na licha ya kuwa bado hatujajibiwa , lakini ofa yetu ipo pale pale,”alisema Rais Putin.
Alisema, anajivunia sana baada ya kusikia katika vyombo vya habari kuwa, Skripal ameruhusiwa kutoka hospitali alipokuwa amelazwa na akamtakia afya njema.
Kachero huyo wa jeshi mwenye umri wa miaka 66 ambaye aliwahi kuhukumiwa nchini hapa kwa tuhuma za kutumiwa na Uingereza na bintiye, Yulia, 33, Machi 4 mwaka huu walikutwa wakiwa katika hali mbaya kwenye benchi lililopo karibu na duka la Maltings mjini Salisbury.