Na ELIZABETH KILINDI-NJOMBE
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) MKoa wa Njombe, imsimamishe kazi meneja miradi wa chuo hicho.
Amesema kwamba, kitendo cha meneja huyo kushindwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa Chuo cha Veta Mkoa wa Njombe, hakitakiwi kufumbiwa macho kwa kuwa mradi huo una thamani ya zaidi ya Sh bilioni tisa.
Akizungumza mwishoni mwa wiki baada ya kutembelea mradi huo uliopo Kijiji cha Shaurimoyo wilayani Ludewa, mkoani hapa, Dk. Ndalichako aliagiza pia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuufanyia uchunguzi mkataba wa mradi huo.
“Taarifa nimezipata na nimeambiwa huyu mkandarasi, Herkin Builder LTD, hawezi kufanya kazi lakini nasikia mlimtetea tetea mpaka akasaini mkataba.
“Kwa hiyo, naagiza bodi ya wakurugenzi imsimamishe kazi meneja miradi hadi uchunguzi dhidi yake utakapokamilika,” alisema Profesa Ndalichako.
Kwa upande wake Mkandarasi wa mradi huo, Steven Mwakasasa, alitaja sababu za kuchelewa kukamilika kwa mradi huo, kuwa ni pamoja na gharama za kuanzia kuwa ndogo ikilinganishwa na mahitaji halisi.
Awali, akisoma taarifa kwa niaba ya Mhandisi Mshauri, Tumaini Mzuma, karani wa mradi huo alisema mkandarasi anayetekeleza mradi huo hana uwezo wa kuukamilisha kama inavyotakiwa.
Mradi huo wa Veta Mkoa wa Njombe unatekelezwa na Serikali kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) pamoja na fedha za ndani na una majengo 25.