33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

PROF. MUHONGO KUJIKITA NA ELIMU JIMBONI KWAKE

Na SHOMARI BINDA


MBUNGE wa   Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo (CCM), ameeleza kipaumbele chake kwa sasa katika jimbo lake kuwa ni elimu kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo wa yote.

Alikuwa akizungumza juzi katika Kijiji cha Muhoji wakati wa ziara yake jimboni kufuatilia na kuhamasisha shughuli za maendeleo.

 Muhongo alisema elimu ni muhimu katika kusukuma maendeleo na   kwa sasa nguvu yote ni wanafunzi kusoma.

Alisema kusomesha vijana ni uwekezaji mzuri kwa vile baadaye watakuja kusaidia masuala ya maendeleo jimboni na Tanzania kwa ujumla.

Mbunge huyo alisema kwa sasa kasi kubwa ni kuhakikisha elimu inasimama kwa kuwa shule nyingi zimekuwa zikifanya vibaya.

Muhongo alisema ni aibu kwa shule   jimboni humo kufanya vibaya kwa sasa wakati katika miaka iliyopita wasomi wengi wengi wamekuwa wakitoka ukanda huo ambao wamekuwa wakishika nafasi mbalimbali za uongozi katika taifa.

"Tuone aibu kwa kiwango cha elimu kwa sasa kwa kuwa shule zetu zimekuwa zikifanya vibaya na lazima kila mmoja achukue hatua ya kuhakikisha elimu inasonga mbele na kuibua wasomi wengi.

"Kwa sasa mimi kipaumbele changu ninachokwenda nacho ni elimu … kuna watu wanakuja na maombi mengine lakini mimi naona twende kwanza na elimu na hayo mengine tutakuja kuyafanya baadaye," alisema Muhongo.

Alisema tayari amefikisha vitabu 20,000 jimboni vikiwamo vya sayansi   na mifuko ya saruji 1,269 na mabati 5,120 kwa ajili ya kupunguza uhaba wa vyumba vya madarasa   wanafunzi waweze kupata sehemu sahihi ya kupata elimu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Charles Magoma, alisema Profesa Muhongo anafanya jitihada kubwa za kuhamasisha masuala ya elimu jimboni hivyo  atahakikisha  anaunga mkono jitihada zote anazozifanya.

Nao wananchi walisema wataendelea kuweka nguvu zao hususan kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa   kupunguza uhaba uliopo na wanafunzi wakae madarasani kwa kuwa kwa sasa wapo wanaosomea chini ya miti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles