Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli amefanya uteuzi wa wabunge wawili na balozi mmoja.
Wabunge walioteuliwa ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo na Profesa Palamagamba Kabudi ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha Sheria.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kuwa wabunge hao wateule wataapishwa kwa taratibu za Bunge.
Rais Magufuli pia amemteua Benedicto Mashiba kuwa balozi.
Kituo cha kazi na tarehe ya kuapishwa kwa Balozi Mteule Mashiba itatangazwa baadaye.
Rais Dk. Magufuli amewateua kuwa wabunge kupitia viti 10 vya Rais ambavyo anaweza kumteua mtu yeyote anayeona anafaa kuwa mbunge kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hadi sasa kiongozi huyo wa nchi ameshafanya uteuzi wa wabunge saba kwa nafasi yake.
Novemba 16, mwaka juzi, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Naibu Mwanasheria Mkuu, Dk. Tulia Ackson na kumteua kuwa Mbunge.
Desemba 10, mwaka juzi, Rais Dk. Magufuli, aliwateua kuwa wabunge, Dk. Possi Abdallah, Balozi Dk. Augustino Mahiga, Profesa Makame Mbarawa, Profesa. Joyce Ndalichako na Dk. Philip Mpango ambao aliwateua kuwa mawaziri na naibu waziri.