Na ZAINAB IDDY, DAR ES SALAAM
UONGOZI wa Tanzania Prisons, umeanika ripoti ya msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara, iliyowasilishwa kwao na kocha wao Aldof Rishard huku kipaumbele kikiwa kuboresha eneo la ushambuliaji.
Prisons ilikuwa kwenye wakati mgumu mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kutokana na kupoteza michezo mingi, lakini ilizunduka mzunguko wa pili na kuepuka kushuka daraja, baada ya kumaliza nafasi ya 12 ikiwa na pointi 46.
Akizungumza na MTANZANIA, Katibu Mkuu wa Prisons, Ajabu Kifukwe, alisema katika ripoti hiyo, Rishard amewataka kuhakikisha wanasajili washambuliaji wanne wenye ubora mkubwa kuliko walionao sasa.
“Msimu uliopita hatukuweza kufanya vizuri kwani mzunguko wa kwanza tulishinda mechi moja tu jambo, ambalo lilituweka katika hatari ya kushuka daraja, kitu hiki hatutaki kijirudie tena ligi ijayo.
“ Kilichotokea msimu uliopita ni funzo kwetu, tutahakikisha haturudii makosa, tutaifanyia kazi ripoti ya mwalimu ambayo amekazania zaidi katika nafasi ya ushambuliji,”alisema.