KAMATI ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kilimanjaro, ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla, imetekeketeza pombe haramu ya gongo lita 140, mitambo sita na mapipa 33 yenye malighafi ya kutengenezea pombe hiyo, katika Kijiji cha Kikelelwa wilayani Rombo.
Akizungumza wakati wa kuteteketeza pombe hiyo, Makala alisema Wilaya ya Rombo inaongoza kwa kutengeneza pombe za kienyeji zaidi ya 50 kwa kutumia kemikali ambazo ni hatari kwa afya za binadamu.
Alisema kemikali zinazotumika kiutengeneza pombe hizo haramu ni pamoja na mbolea ya urea, kinyesi cha binadamu, unga wa betri, sukari guru na molasesi.
“Hii ni hatari ndugu zangu hatuwezi kujenga Taifa kwa njia hii, pombe haramu haikubaliki na hupoteza nguvu kazi ya Taifa, leo tumetekeza pombe hizi na kazi hii itakuwa ya kudumu na vyombo vya ulinzi vipo macho wakati wote.
“… wale watakaobainika kuendelea na biashara hii ya pombe haramu pamoja na mambo mengine ambayo ni kinyume cha sheria, watatiwa mbaroni tu,” alisema Makalla.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho kilichopo mpakani mwa Tanzania na Kenya, walisema utengenezaji wa pombe hiyo imeleta madhara makubwa kwa wananchi wa Rombo hususan vijana hali ambayo inasababisha wanawake wengi kubeba mzigo wa kuhudumia familia.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Tarakea Motamburi, Nicodemas Kimaro, alisema kazi ya ukamaji wa pombe haramu ilianza Januari mwaka huu.
“Pamoja Serikali kupiga marufuku utengenezaji wa pombe haramu zote ikiwamo gongo lakini bado kuna baadhi ya watu wamekuwa wakikaidi amri hii,” alisema Kimaro