22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga, Simba, Azam jino kwa jino

1NA ZAITUNI KIBWANA, DAR ES SALAAM

TIMU ya Yanga imezidi kujikita kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuinyuka timu ya JKT Ruvu mabao 4-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana.

Yanga walianza kufanya mashambulizi ikiwa ni dakika ya kwanza baada ya Malimi Busungu kushindwa kumfunga kipa wa JKT Ruvu, Shaban Dihile kwa kichwa na kudaka kufuatia pasi ya Juma Abdul.

JKT Ruvu nao walifanya shambulizi katika dakika ya tatu lakini walipoteza nafasi ya kufunga baada ya Paul Mhidze kushindwa kufunga kutokana na pasi ya Mussa Juma, lakini kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’ alipangua shuti lake.

Yanga waliandika bao la kwanza katika dakika ya 12 lililofungwa na mshambuliaji Simon Msuva baada ya kuuwahi mpira uliorushwa na Abdul na kupiga shuti la mbali lililomshinda kipa Dihile.

Katika dakika ya 15, Haruna Niyonzima aliingiza krosi kati na kutua kichwani kwa Msuva, lakini alishindwa kufunga baada ya Dihile kudaka.

Yanga walijipatia bao la pili katika dakika ya 44 lililofungwa na Issoifou Boibacar Garba baada ya kumalizia pasi ya Msuva.

Yanga walipoteza nafasi ya kufunga katika dakika ya 51 baada ya Paul Nonga aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Busungu kushindwa kufunga baada ya kupiga shuti hafifu lililookolewa na Dihile.

Donald Ngoma aliifungia Yanga bao la tatu kwa kichwa katika dakika ya 63 baada kumalizia kazi ya Abdul na kumfanya akifikishe mabao 10.

Katika dakika ya 77, Yanga walipoteza nafasi nyingine ya kufunga baada ya kupiga shuti ambalo liliokolewa na Dihile.

Yanga waliongeza bao la nne katika dakika ya 90 lililofungwa na Msuva kwa shuti kali baada ya kutanguliziwa mpira na Nonga.

Mahasimu wao timu ya Simba nayo iliendeleza wimbi la ushindi katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga baada ya kuifunga Kagera Sugar bao 1-0.

Bao hilo pekee la Simba lilifungwa katika dakika 44 kupitia kwa Ibrahim Ajib kwa shuti.

Simba wameendelea kuweka rekodi nzuri baada ya kushinda mfululizo michezo sita tangu Jackson Mayanja alipoanza kuifundisha timu hiyo akichukua mikoba ya Dylan Kerr.

Timu hiyo imepata ushindi katika michezo mitano ya Ligi Kuu huku ikishinda mabao 3-0 dhidi ya Burkina Faso kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho (FA) uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 42 sawa na Azam FC.

Simba itabidi wajilaumu baada ya Ajib kukosa penalti katika dakika ya 84  kufuatia kuangushwa katika eneo la hatari.

Nayo Azam FC wameifunga Mwadui FC bao 1-0 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Bao hilo la Azam lilifungwa na mshambuliaji Kipre Tchetche katika dakika ya 19.

Katika mchezo mwingine, Toto African ya Mwanza imeichapa Coastal Union ya Tanga mabao 2-1 katika Uwanja wa CCM Kirumba.

Toto walianza kupata bao la kwanza katika dakika ya 43 kupitia kwa Jamla Mtengeta baada ya kumalizia kazi ya Miraji Makka.

Coastal Union walisawazisha bao hilo dakika ya 50 kupitia kwa Juma Mahadhi kwa shuti la mbali lililomshinda kipa wa Toto Africans, Erick Ngwe’ngwe.

Hata hivyo, Toto Africans waliongeza bao la pili katika dakika ya 75 lililofungwa na Edward Shija baada ya kumalizia pasi ya Jafari Mohamed.

Katika mchezo mwingine uliochezwa katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Mbeya City walitoka uwanjani bila kufungana na ndugu zao wa Tanzania Prisons.

Katika mchezo mwingine, timu ya Ndanda FC imetoka sare ya kufungana bao 1-1 na Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Majimaji nao wakicheza nyumbani katika Uwanja wa Majimaji, Songea mkoani Ruvuma, waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mgambo JKT.

 

JKT Ruvu: Shaban Dihile, Michael Aidan, Paul Mhidze/ Abdulrahman Mussa, Nurdin Mohamed, Madenge Ramadhan, Naftar Nashon, Mussa Juma, Hassan Dilunga, Gaudence Mwaikimba/Hamis Shengo, Samwel Kamuntu na  Emmanuel Pius/ Amos Edward.

Yanga: Ally Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Vicent Bossou, Salum Telela, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma/Geofrey Mwashuiya, Malimi Busungu/Paul Nonga na Issoifou Boubacar Garba/ Deus Kaseke.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles