25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI WAZUIWA KUKAMATA WATUHUMIWA NJE YA MAHAKAMA

Na KULWA MZEE -MOROGORO       |       

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, imezuia kamatakamata inayofanywa na polisi katika viunga vya mahakama, muda mfupi baada ya mshtakiwa ama washtakiwa kuachiwa kwani kitendo hicho kinafedhehesha.

Hayo yalisemwa jana mjini hapa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Morogoro, Elizabeth Nyembele katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, alipokuwa akitoa mafunzo ya vitendo kwa wahariri na waandishi wa habari za mahakamani nchini.

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania kupitia Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na kufadhiliwa na Benki ya Dunia.

“Tumezungumza na wadau husika wote, tumewaambia polisi wasiendelee kuwakamata washtakiwa mara wanapoachiwa kwa mujibu wa sheria mahakamani.

“Kuna wakati kesi inakuwa na upungufu wa kisheria, mahakama inaamua kuifuta kwa kifungu ambacho washtakiwa wanaweza kukamatwa tena… polisi wanavizia, washtakiwa wakitoka tu wanawakamata na wakati mwingine mbele ya hakimu.

“Washtakiwa nao wakiachiwa wanawaza kukimbia, vitendo hivi vinaweza kusababisha madhara, askari kama hajui anayekimbia kaachiwa, anaweza kufyatua risasi ikamdhuru mshtakiwa au mtu mwingine yeyote.

“Mahakimu wakati unataka kuwaachia washtakiwa unatakiwa kuwapa elimu kwamba nakuachia kwa kifungu hiki, lakini unaweza kufunguliwa kesi nyingine, washtakiwa ni wastaarabu, wanaelewa wala hawawezi kukimbia,” alisema.

Utaratibu wa polisi kukamata washtakiwa mara tu baada ya kuachiwa chini ya kifungu cha Sheria ya Makosa ya Jinai 225, kimekuwa kikilalamikiwa kwa muda mrefu, kimekuwa kikifanywa mara kwa mara katika mahakama zetu.

Katika hatua nyingine, Hakimu Nyembele alisema Mahakama Mkoa wa Morogoro inaongoza kwa kuwa na kesi nyingi za unyang’anyi, dawa za kulevya na ujangili kwa sababu wamezungukwa na mbuga nyingi.

Akizungumzia changamoto zilizopo katika mahakama hiyo, alitaja ufinyu wa chumba cha mahabusu na jengo la mahakama.

“Lakini hayo yote yanakaribia kumalizika kwani kuna jengo kubwa linajengwa maeneo ya Kihonda.

“Changamoto nyingine ni mashahidi, wengine wanatokea vijijini, malipo yao huyapata wakishafika mahakamani, lakini namna ya kutoka huko walipo ni tatizo, unakuta mwingine anakwambia nauli ya kumfikisha mahakamani hana, anakwambia anatafuta na wakati mwingine shahidi anatoka Mahenge, nauli Sh 30,000,” alisema.

Mtendaji Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Nestory Mujunangoma, alisema jengo jipya la mahakama litakuwa na ghorofa nne na litakuwa na Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Mkoa, Mahakama Kuu na kutakuwepo na chumba kwa Mahakama ya Rufaa.

“Tunatarajia kuhamia katika jengo hilo ifikapo 2020, kuanza kutumika kwa jengo hilo kutamaliza changamoto zote zilizopo, idadi ya watendaji itaongezeka pamoja na mahakimu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles