Raphael Okello -Bunda
WAKATI Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2019 ukiwa ni wa kwanza katika Halmashauri ya mji wa Bunda tangu ilipotengwa rasmi, vyombo vya dola vimeeleza bayana kuanza kujipanga kwa ajili ya kuhakikisha uchaguzi huo unatawaliwa na amani.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Bunda mkoani Mara, Hamisi Waryoba amesema atahakikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu wilayani Bunda unakuwa huru na haki.
Alisema hatamwonea mtu yeyote hivyo amewataka wote watakaojihusisha katika masuala ya uchaguzi kufuata sheria, kanuni na taratibu zote za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 kama zilivyoanishwa katika mwongozo.
Waryoba alisema hayo juzi alipokuwa akijitambulisha kwa madiwani nawatendaji katika baraza la madiwani la Halmashauri ya Mji wa Bunda ambapo alisema uchaguzi ni shughuli nyeti inayowaletea wananchi viongozi bora waliowachagua wao wenyewe hivyo ni vyema ufanyike katika mazingira huru na haki.
Alisema anao uzoefu wa kutosha katika historia ya wilaya ya Bunda hivyo wakazi wa eneo hilo wasiwe na hofu na kwamba yeye ni muumini wa polisi shirikishi (polisi jamii) na  ameomba ushirikiano mkubwa toka kwa jamii.
Tayari msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Wiliam Wakili ametangaza jumla ya mitaa 88 katika kata 14 za Halmashauri ya Mji wa Bunda ambayo wananchi wake watashiriki katika uchaguzi kupata viongozi wa serikali za mitaa yao.
Awali Mbunge wa kitaifa kutoka Mkoa wa Mara, Amina Makilagi aliwataka wanawake wenye sifa kuwania nafasi hizo za uongozi katika serikali za mitaa.
Alisema nafasi hizo ziko wazi kwa raia yeyote wa Tanzania mwenye sifa kugombea bila kujali jinsia, rangi, dini au kabila huku akisema akina mama wanayo nafasi kubwa kuchaguliwa kwa kuwa wana nguvu kubwa katika jamii.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 unakuwa ni uchaguzi wa kwanza katika halmashauri ya mji wa Bunda tangu  halmashauri hiyo itengwe rasmi kutoka halmashauri mama ya Wilaya ya Bunda na kupata madiwani na mbunge katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Mwaka 2016 wenyeviti wa vitongoji waliochaguliwa katika uchaguzi waserikali za mitaa mwaka 2014 walisitishwa kufanyakazi kwa mujibu wa sheria za Serikali za Mitaa na Halmashauri ya miji huku usimamizi wa shughuli zote za kiuwakilishi zikiachwa kwa madiwani.