28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Pluijm alalamika Yanga

plujimJENNIFER ULLEMBO NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

IKIWA imebaki siku moja kabla ya kikosi cha Yanga kushuka dimbani kukabiliana na Cercle de Joachim ya Mauritius katika mchezo wa marudiano wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika, Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Hans van der Pluijm amelalamikia kiwango kibovu kilichoonyeshwa juzi na wachezaji wake katika mchezo wa Kombe la FA dhidi ya JKT Mlale, jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo wa kimataifa unaotarajiwa kufanyika Uwanja wa Taifa, Yanga inatakiwa kushinda au kutoka sare ili iweze kuingia raundi ya kwanza, ambapo katika mchezo wa awali uliochezwa nchini Mauritius iliweza kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Akizungumza  jijini Dar es Salaam juzi, mara baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi  JKT Mlale na kikosi chake kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, Pluijm alisema licha ya ushindi walioupata, kiwango cha wachezaji wake hakijamridhisha.

Pluijm alisema umefika wakati wachezaji wake kubadilika na kuheshimu mashindano yote, bila kuangalia ukubwa wa timu wanazokutana nazo.

“Tumeshinda, lakini kiwango hakijanifurahisha, wachezaji wamecheza hovyo na sababu kubwa ni kudharau timu au mchezo kwa ujumla, lazima waonyeshe mabadiliko, hasa kipindi hiki tunachoelekea kwenye mchezo wa kimataifa.

“Hakuna timu ndogo, kila timu ina ufundi wake na mbinu za kupata  ushindi, sidhani kama wachezaji wangu watarudia makosa yaliyojitokeza juzi katika mchezo wa kesho,” alisema.

Pluijm alieleza anatambua Cercle de Joachim wanakuja nchini wakiwa na dhamira ya kulipiza kisasi, hivyo lazima wajitume na kuonyesha uwezo zaidi kama wana malengo ya kusonga mbele katika michuano hiyo ya kimataifa.

Yanga itakabiliana na Cercle kesho, huku ikiwakosa wachezaji wake nyota, Haruna Niyonzima, Salum Telela na Donald Ngoma.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Habari cha klabu hiyo, Jerry Muro, Niyonzima anauguza kifundo cha mguu, huku Telela akisumbuliwa na nyama za paja.

Muro alisema upande wa mchezaji wao Ngoma, alitarajiwa kuondoka nchini jana kuelekeza Zimbabwe, baada ya kupata msiba wa mdogo wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles