NA BEATRICE KAIZA
STAA wa muziki wa Bongo Fleva, Benald Paul ‘Ben Pol’, ameingia kwenye orodha ya wasanii wanaopiga picha zenye utata mkubwa na kusababisha mjadala kwenye mitandao ya kijamii.
Ben Pol aliweka picha kwenye mtandao wake wa Instagram akiwa nusu utupu, amekaa kwenye kiti na mikono yake ikiwa imefungwa kamba.
MTANZANIA lilimtafuta msanii huyo kwa njia ya simu ili kujua nini kimemkuta hadi kuamua kupiga picha hizo ambazo zimeleta mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, lakini alipokea na kujibu: “Nipo kwenye kikao kwa sasa siwezi kuongea chochote.”
Hata hivyo, hadi gazeti linaingia mtamboni halikuweza kufanikiwa kupata maelezo kutoka kwake. Lakini mashabiki wamekuwa na mawazo tofauti huku wengine wakiamini kuwa msanii huyo mpole atakuwa na wimbo wake mpya ambao anataka kuutoa na ndio maana ameposti picha hizo tatu.
Imekuwa kama ni staili kwa wasanii wa hapa nyumbani wakitaka kutoa kazi zao mpya wanatafuta kiki mbalimbali ili kusaidia nyimbo zao kufanya vema.