NEW YORK, MAREKANI
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amekubali uamuzi wa kujiuzulu wa Kardinali wa Marekani, Theodore McCarrick kutoka Baraza la Makardinali kutokana na madai ya kumdhalilisha kingono mvulana wa miaka 11.
Kiongozi huyo alichukua hatua haraka mara tu baada ya kupokea barua ya kujizulu ya McCarrick hapo juzi.
Juni mwaka huu, Askofu huyo wa Washington alivuliwa mamlaka ya ukasisi baada ya uchunguzi kubainisha palikuwapo ushahidi thabiti kuonyesha kuwa alimdhalilisha mvulana huyo.
McCarrik (88) ni miongoni mwa makadinali maarufu duniani na kiongozi wa dini wa ngazi ya juu kuwahi kukabiliwa mashtaka ya udhalilishaji wa kingono .
Hata hivyo, mashtaka hayo yanayotokana na tukio la miaka 40 iliyopita, ambapo anadaiwa alimshikashika mvulana huyu jijini New York kwa kipindi cha miaka miwili.
McCarrik amekanusha madai ya kumdhalilisha mvulana huyo, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 51.
Papa Francis amechukua hatua haraka kutekeleza ahadi aliyotoa ya kutovumilia tabia ya kufichiana siri miongoni mwa makasisi.
Madai ya udhalilishaji wa kingono yanawakabili makasisi wengi ikiwa pamoja na maaskofu na makardinali ikiwa pamoja na Kadinali wa Australia George Pell ambaye ni mmoja wa washauri wa ndani wa baba mtakatifu.