NA ASHA MUHAJI
‘ZEGE halilali’ ndivyo itakavyokuwa leo pale miamba ya soka na wenye utani wa jadi nchini, Yanga na Simba watakapokutana katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, katika mchezo wa Ngao ya Jamii ukiashiria uzinduzi rasmi wa michuano ya ligi kuu msimu huu wa 2017/2018.
Uhondo wa pambano la leo unatokana na ukweli kwamba, ni lazima mshindi apatikane tofauti na mechi za ligi kuu, ambapo matokeo yoyote matatu kati ya kushinda, kufungwa na sare hukubalika.
Timu hizo zimepata tiketi ya kucheza leo baada ya Yanga kuwa Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu wakati Simba ni bingwa wa Kombe la FA.
Awali mechi hiyo ya Ngao ya Jamii ilikuwa ikizikutanisha bingwa wa ligi kuu na mshindi wa pili kabla ya mwaka 2009 kubadilishwa na kukutanisha mabingwa wa ligi na FA.
Ni mechi ambayo hakika haitauacha salama upande wowote ambao utapoteza mchezo huo kutokana na historia ya kimazingira iliyopo baina ya klabu hizo.
Licha ya kwamba mchezo huo si wa Ligi Kuu, lakini ukweli bado unabaki pale pale kuwa wakutanapo watani hao wa jadi, nyasi huwaka moto kwani ushindani baina yao ni mkali, achilia mbali majigambo na vimbwanga kadhaa kutoka kwa mashabiki wao.
Yanga itaingia katika pambano hilo ikiwa na kumbukumbu nzuri zaidi ya mechi hizo, kwani imeshiriki mara nane kati ya tisa ilizofanyika hadi sasa, huku ikibeba Ngao hiyo mara tano wakati Simba wao wameshiriki mara nne na kufanikiwa kutwaa ubingwa huo mara mbili tu.
Mashabiki wa soka wanaamini msimu huu Simba ina kikosi kizuri na bora zaidi ukilinganisha na Yanga ambao wachezaji wake wengi wazuri wameondoka, hivyo kuwa na sura ya kujengwa upya.
Licha ya Simba kusheheni wachezaji wengi maarufu na wenye uzoefu mkubwa ‘wahenga’ dhidi ya Yanga wenye wachezaji wengi wapya na wasio na uzoefu sana wanaoonekana kama ni chipukizi, bado ni vigumu kubashiri upande upi unaweza kushinda kirahisi.
Si rahisi kutabiri mchezo huo kutokana na ukweli kuwa pambano baina ya watani hao wa jadi huwa ni zaidi ya dakika 90 za uwanjani, hivyo msemo wa ‘ukitaka kumchinja kobe ni timing tu’ utahusika sana.
Mashabiki watarajie upinzani mkali baina ya timu hizo ambapo pasi na shaka timu itakayoshindwa basi haitabaki salama, kwani historia inaonesha timu hizo chanzo kikubwa cha migogoro kati ya klabu hizo na makocha wao huanzia katika mechi baina yao.
Je, leo ni kocha yupi ataendeleza historia hiyo kati ya George Lwandamina (Yanga) na Joseph Omog (Simba) kuandaliwa safari ya kurudi kwao?
Inaaminiwa Omog licha ya kuwa na wachezaji wazuri waliosainiwa kwa thamani kubwa, anashindwa nguvu na upana wa kikosi chake hasa baada ya kucheza mechi sita na kushinda michezo mitano, ilipoteza mmoja huku safu yake ya ushambuliaji ikionekana dhahiri kuwa butu.
Yanga inaonekana kuwa na pengo katika safu ya ulinzi, huku upande wa ushambuliaji ikionekana kuwa na uchu wa mabao licha ya kucheza mechi tano za kirafiki, kati ya hizo wameshinda nne na kupoteza moja.
Mchezo utakuwa ni wa 10 katika historia ya Ngao ya Jamii toka ianzishwe mwaka 2001.
Mara ya kwanza ilipofanyika mwaka 2001, iliwakutanisha watani hao wa jadi ambapo Yanga iliyokuwa nyuma kwa bao 1-0 lililofungwa na Steven Mapunda ‘Garincha’, iliweza kusawazisha kupitia kwa Edibily Lunyamila na Ally Yusuph ‘Tigana’ kumalizia kazi kwa kuifungia bao la pili na kufanya matokeo kuwa 2-1.
TFF iliifuta mechi hiyo na kusimama kwa takribani miaka nane kabla ya kuifufua mwaka 2009 na kuwakutanisha watani hao wa jadi, lakini hata hivyo Simba iligomea mchezo huo na kusababisha Mtibwa iliyokuwa ikishika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo kupewa nafasi.
Mtibwa iliweka historia kwa kushiriki kwa mara ya kwanza na kufanikiwa kutwaa ubingwa huo baada ya kuilaza Yanga kwa bao 1-0 lililofungwa na Pius Kisambale.
Katika msimu uliofuata wa 2010, Ngao hiyo iliwakutanisha tena watani hao na Yanga kuibuka kidedea kwa mikwaju mitatu ya penalti dhidi ya moja ya wapinzani wao, baada ya kwenda sare katika muda wa kawaida. Penalti za Yanga zilifungwa na Godfrey Bonny, Stephano Mwasika na Isack Boakye wakati Mohammed Banka, Emmanuel Okwi, Uhusru Selemani na Juma Nyoso walikosa kwa upande wa Simba.
Ngao hiyo iliwapenda tena watani hao na mwaka 2011 Simba walitwaa ubingwa kwa mara ya kwanza, baada ya kushinda kwa mabao 2-0, wafungaji wakiwa ni Haruna Moshi ‘Boban’ na Felix Sunzu.
Msimu wa 2012, Simba ilishinda mabao 3-2 dhidi ya Azam. Mabao yakifungwa na Daniel Akufor, Emmanuel Okwi na Mwinyi Kazimoto wa Simba, huku yale ya wapinzani wao yakifungwa na John Bocco na Kipre Tcheche.
Yanga walizinduka na kutwaa ngao hiyo msimu wa 2013 kwa bao pekee la kiungo Salum Telela lililoizamisha Azam. Mwaka 2014 Yanga ikatembeza tena ubabe dhidi ya Azam na kutwaa ubingwa huo kwa jumla ya mabao 3-0, huku Geilson Santos ‘Jaja’ akipachika mabao mawili na Simon Msuva akiweka kimiani moja.
Msimu wa 2015 ilizikutanisha tena Yanga na Azam na matokeo kuwa sare ya bao 1-1, hivyo kupigiana penalti ambapo Wanajangwani hao waliibuka kidedea kwa  mikwaju nane dhidi  ya saba ya wapinzani wao.
Mikwaju ya Yanga ilifungwa na Niyonzima, Kaseke, Geofrey Mwashiuya, Amis Tambwe, Andrey Coutinho, Thaban Kamusoko, Mbuyu Twite na Kelvin Yondani, wakati ile ya wana-Lambalamba ilipachikwa na Kipre, Bocco, Himid Mao, Aggrey Moris, Jean Baptiste Mugiraneza, Erasto Nyoni na Shomari Kapombe.
Katika mchezo kama huo uliofanyika mwaka jana, Azam walitwaa Ngao baada ya kuifunga Yanga kwa mikwaju minne ya penalti dhidi ya moja ya wapinzani wao kufuatia sare ya mabao 2-2.