BONDIA Manny Pacquiao anaweza kufungiwa au kupigwa faini na viongozi wa Kamisheni ya Ngumi Nevada kwa kushindwa kuweka wazi majeraha ya bega kabla ya pambano lake dhidi ya Floyd Mayweather Jr.
Alfajiri ya Jumapili Mfilipino huyo alipigwa na Mayweather kwa pointi kwenye pambano la karne lililofanyika Las Vegas, lakini baadaye Pacquiao alisingizia alipata maumivu ya bega mazoezini yaliyomfanya kushindwa kutumia vema mkono wake wa kushoto.
Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo, Francisco Aguilar, alisema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya nchi hiyo inachunguza kwanini Pacquiao alisema ‘hapana’ kama hana maumivu ya bega kwenye karatasi ya maswali aliyopewa siku moja kabla ya pambano hilo.
“Tutakusanya ushahidi wote kuhusu suala hilo na kuangalia mazingira yake,” alisema Aguilar. “Wakati fulani tutakuwa kwenye mazungumzo. Kwani ukiwa kama mtoa leseni unatakiwa kupata taarifa za mara kwa mara kutoka kwa mabondia.”
Pacquiao anaweza kutozwa faini au kufungiwa kutokana na kushindwa kujibu maswali kwa usahihi kwenye fomu aliyopewa, ambayo aliijaza kabla ya zoezi la upimaji uzito Ijumaa iliyopita.
Wakati huo huo, Daktari wa Mifupa na Upasuaji, Neal ElAttrache, ameuambia mtandao wa ESPN.Com kuwa Pacquiao atafanyiwa upasuaji wa bega baadaye wiki hii kwa ajili ya kutibu jeraha lake hilo.
Neal Alattrache amesema, bondia huyo anatarajia kufanyiwa upasuaji wa bega hilo baada ya kufanyiwa vipimo ambapo atakaa nje ya uwanja kwa muda wa miezi sita, huku akitakiwa kukaa miezi tisa bila pambano.
“Kama atafanikiwa kufanyiwa upasuaji atatarajia kuanza mazoezi baada ya miezi sita…Kutokana na hali hiyo anatakiwa kuwa mvumilivu kwa kipindi hicho chote ili aweze kuwa fiti, atatakiwa kuanza kupigana baada ya miezi tisa baada ya kufanyiwa upasuaji,” alisema.