23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ni pigo la nchi

MTZ Alhamisi new july.inddMwandishi Wetu na Mashirika ya Kimataifa
ASKARI wawili wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanaolinda amani katika Kikosi cha Umoja wa Mataifa (MONUSC) nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wameuawa na waasi.
Askari hao ambao majina yao hayajatambuliwa, waliuawa juzi alasiri katika shambulio la kushtukiza mashariki mwa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa jana na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kupitia msemaji wa MONUSCO, Kanali Felix Basse, ilisema mbali ya waliouawa, wanajeshi wengine 13 walijeruhiwa na wanne hawajulikani waliko.
Shambulio hilo lilitokea wakati wanajeshi hao wakiwa katika doria ya kawaida katika Kijiji cha Kisiki, ambako vikosi vya Serikali ya DRC vinapambana na waasi wa Uganda wenye itikadi kali ya Kiislamu – ADF.
Kijiji hicho kipo umbali wa kilomita 50 kaskazini mwa mji wa Beni katika Jimbo la Kivu ya Kaskazini.
Taarifa zinasema askari hao walipofika katika kijiji hicho walikuta waasi wamejificha pande mbili za barabara.
Kutokana na hali hiyo, walijikuta wakishambuliwa kwa silaha nzito kutoka kila upande jambo ambalo liliwapa wakati mgumu kujibu mashambulizi.
Nalo Shirika la Habari la Ujerumani (Deutsche-welle) katika matangazo yake ya saa saba mchana jana, lilisema waasi hao wamefanya shambulizi hilo kwa madai ya kulipa kisasi cha kiongozi wao kukamatwa na vyombo vya dola vya Tanzania.
Mmoja wa watu walihojiwa alisema: “Waasi walinipiga risasi wakanivunja mguu, mimi ni dereva teksi… sababu kubwa ya kufanya mashambulizi haya wanadai kiongozi wao kakamatwa na Tanzania.
“Walikuwa wamefunga eneo lote la barabara, wana silaha nzito… sijui hata abiria niliokuwa nao wako hai ama la,” alisema mtu huyo.
Juzi, jeshi la DRC lilisema limewaua wapiganaji 16 wa ADF wakati wa mapambano makali katika eneo hilo mwishoni mwa wiki iliyopita.
Shambulizi hilo ni la pili dhidi ya vikosi vya Umoja wa Mataifa (UN) ndani ya saa 48, baada ya helikopta ya MONUSCO kushambuliwa na watu wasiojulikana siku ya Jumatatu.
Mkuu wa operesheni za MONUSCO, Martin Kobler, alilaani shambulio hilo dhidi ya kikosi cha wanajeshi wa Tanzania kinacholinda amani katika kijiji hicho.
Jeshi la DRC lilizindua ‘Operesheni Sukola’ dhidi ya ADF mwaka jana, baada ya kundi hilo kutuhumiwa kuua wanakijiji 300 karibu na mji wa Beni kati ya Oktoba na Desemba mwaka jana.
Umoja wa Mataifa upo katika harakati za kuvunja makundi kadhaa ya waasi mashariki mwa DRC, baada ya miongo miwili ya mgogoro ambao sehemu kubwa umechochewa na utajiri wa madini.
Naye Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon amelaani shambulio hilo na kuonya umoja huo hautavumilia kurudiwa tena kwa vitendo vya kushambulia watu wenye dhamana na maisha ya raia.
“Nimesikitishwa na tukio hili, hatutakuwa tayari kuona watu waliopewa dhamana ya kusimamia maisha ya watu wanauawa hivi…tutachukua hatua,” alisema Ki-moon.
Agosti, mwaka jana askari wa Tanzania, Luteni Rajabu Ahmed Mlima aliuawa, huku wengine watano raia wa Afrika Kusini wakijeruhiwa katika mapigano na waasi wa kundi la M23 mashariki mwa DRC.
Msemaji wa vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini humo, Madnodje Mounoubai, alisema askari huyo aliuawa katika mapigano wakati waasi walipokuwa wakipambana na wanajeshi wa Serikali ya DRC.
Mapigano hayo yalitokea karibu na Goma, mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini.
Jeshi la DRC linapata msaada wa kikosi cha askari 3,000 wa Umoja wa Mataifa ambao wana idhini maalumu ya kupigana ana kwa ana na makundi ya waasi wenye silaha katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini. Kikosi hicho kinajumuisha wanajeshi wa Tanzania, Malawi na Afrika Kusini.

MSEMAJI JWTZ
Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Masanja, alipoulizwa kuhusu tukio hilo alikiri kulisikia.
“Ndugu yangu na mimi nimesikia jambo hili kwenye taarifa ya habari ya redio mchana huu (jana)… naomba mtupe muda tunalifanyia kazi, leo nitawapa taarifa kamili,” alisema Meja Masanja.
Ushiriki wa Tanzania katika Operesheni ya ulinzi wa amani nchini DRC, unatokana na mgogoro kati ya Serikali DRC na waasi hususan kikundi cha waasi cha M23.
Mgogoro huo ulianza Aprili 2012 ambapo kikundi cha M23 kilijitoa katika Jeshi la serikali ya DRC na kuanzisha mapigano hali iliyopelekea hali ya usalama nchini DRC kuwa mbaya.

Kutokana na hali mbaya ya usalama, wakati wa kikao cha International Conference on the Great Lakes Region kilichofanyika tarehe Julai 12, 2012 mjini Addis Ababa, Ethiopia, Rais Joseph Kabila aliwasilisha ombi kwa wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu ambazo Rwanda, Uganda, Tanzania, na DRC akaomba nchi wanachama zisaidie kuwapokonya silaha waasi wa M23.
Pamoja na hali hiyo JWTZ imekuwa ikipata heshima katika Bara la Afrika ambapo askari wake wamekuwa wakilinda amani katika mji wa Darfur nchini Sudan.
Kutokana na kuthaminiwa huko kwa kazi ya JWTZ, hivi karibuni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Dk. Nkosanzana Dlamini Zuma, alimteua Brigedia Jenerali Sara Thomas Rwambali kutoka jeshi hilo kuwa Mwakilishi Maalumu na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Afrika Sudan ya Kusini.
Tangu miaka ya 1960 hadi mwaka 1994 Tanzania kupitia JWTZ imekuwa ikipata heshima ikiwamo kuongoza Kamati ya Ukombozi ya uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ambapo ilikuwa ikihangaika kuzikomboa nchi zote za Kusini mwa Afrika ili zipate uhuru wake.
Hata baada ya kupatikana kwa uhuru wa nchi hizo lakini bado Tanzani ilikuwa ikiongoza mazungumzo ya kutafuta amani kwa nchi za Afrika zikiwamo Burundi na DRC, ambayo hadi sasa bado imekuwa na matukio ya vikundi vya waasi hasa mashariki mwa nchi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles