25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Mgogoro mpya wamiliki mabasi, madereva waibuka

mabasiNa Waandishi Wetu, Dar es Salaam
MGOGORO mpya umeibuka kati ya wamiliki wa mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani baada ya wamiliki kutishia kuwafukuza kazi madereva wao walioshiriki mgomo.
Hatua hiyo imekuja baada ya baadhi ya madereva walioshiriki katika mgomo huo wa siku mbili kufukuzwa kazi na baadhi ya wamiliki wa mabasi hayo.
Kutokana na hatua hiyo, Mhasibu Mkuu wa Umoja wa Madereva Tanzania (UWAMATA) Issa Regan, aliwataka matajiri waliowafukuza madereva wao kuwarudisha kazini mara moja, vinginevyo watawaambia madereva wote wa kampuni husika wagome.
Regan alisema kuwa makosa ya mgomo huo wa juzi si wa madereva, bali uliitishwa na chama chao na wao walitii amri ya viongozi wao.
Regani alimtaja dereva aliyefukuzwa kazi na mmiliki wake kuwa ni Seif Kitumbo wa basi la Kampuni ya Osaka linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Musoma.
Akizungumzia kufukuzwa kwake, Kitumbo alisema chanzo chake ni mgomo ambapo kabla ya kufukuzwa tajiri wake alimwambia kuwa amemsababishia hasara kubwa.
“Nimefanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja na miezi 11 sijawahi kusababisha ajali yoyote, mgomo ulinikuta nikiwa Geita, bosi wangu alinipigia simu na kuniambia niache gari yake na alinipatia Sh 50,000 tu, alisema Kitumbo.
Akizungumzia hatua hiyo Regan alisema. “Nasikitika kwa kitendo hicho na kama hawa matajiri wanataka vita basi tupo radhi kufanya hivyo, lakini sisi tunataka kujenga mahusiano mazuri kati ya madereva na mabosi wao, madai yetu ni ya msingi sijui watu wanaoshindwa kuelewa wanatutaka nini”alihoji Regan.
Naye Katibu Mkuu wa UWAMATA, Abdala Lubala alisema kilichomkuta Kitumbo ni matokeo ya kutokuwa na mikataba kazini kwani kama Kitumbo angekuwa na mkataba asingeweza kufukuzwa kwa staili hiyo.
“Tutahakikisha huyu mwenzetu anapata haki yake hata kurudishwa kazini, tutafuata sheria na hata kwenda mahakamani” alisema.
AMRI YA KURUDI SHULE YAFUTWA
Katika hatua nyingine, Lubala alisema wanashukuru kwani tayari baadhi ya madai yao yamefanyiwa kazi na Serikali.
Alisema lile sharti la madereva kurudi shule kila baada ya miaka mitatu, hivi sasa limeondolewa.
“Baada ya kikao cha jana (juzi)tuliondoka na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda hadi kwa Waziri Mkuu ili kushughulikia masuala ambayo tulikuwa tunayalalamikia pamoja na kujua tume iliyoundwa.
“Tulikuwa pia na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta tulikuta tayari kero ya kurudi shule imeondolewa kimaandishi kama ambavyo tuliomba,” alisema.
Kuhusu muundo wa tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ili kuchunguza madai yao, alisema itajumuisha makatibu wakuu wa wizara nne pamoja na taasisi mbalimbali zinazohusiana na mambo ya usafirishaji.
Alitaja Wizara hizo ni pamoja na Ujenzi, Uchukuzi na Kazi na Ajira.
Wadau wengine ni Chama Cha Wamiliki wa Malori (TATOA), Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Chama cha Madereva (UWAMATA) pamoja na Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (CHAKUA).
“Chama cha Madereva tumepatiwa nafasi tano za wajumbe ndani ya kamati hiyo leo (jana) tumekutana ili kuwateua wawakilishi wetu, kamati itakapoanza kazi itashughulikia suala la mikataba ndani ya siku 30.
Taboa
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) Enea Mrutu, aliliambia MTANZANIA Dar es Salaam jana kuwa uongozi wa chama utawachukulia hatua madereva wote walioshiriki mgomo huo aliosema ni haramu.
Alisema wamiliki hao wanapanga kukutana katika kikao cha dharura ili kujadili mgomo huo, ikiwa ni pamoja na kupanga namna watakavyofanya kazi na madereva ambao watakuwa na maelewano mazuri na serikali pamoja na wamiliki.
Katika kikao hicho alisema pia watajadili hasara waliyoipata kutokana na mgomo huo wa siku mbili mfululizo.
CHAKUA WATOA WITO
Katibu Msaidizi wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), Godwin Ntongeji alitoa wito kwa wamiliki wa mabasi kutochukua nauli kwa abiria iwapo wanajua madereva wao watafanya mgomo.
Aliwataka wamiliki hao kufunga kabisa vituo vyao ili abiria wasikate tiketi kuliko kuwasababishia usumbufu kama uliotokea.
AJIFUNGULIA KITUONI
“Kutokana na adha ya mgomo huo, Ntongeji alisema mwanamke mmoja mjamzito alipatwa na uchungu ghafla usiku ambapo wanawake wenzake walimsaidia akajifungua salama na baadaye alikimbizwa hospitali. Hata hivyo jina la mwanamke huyo halikuweza kujulikana mapema.
MADEREVA WA MALORI
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Malori (Chamamata), Clement Masanja, alisema watawashtaki wamiliki wote ambao watawafukuza madereva wao kwa sababau ya mgomo.
Alisema kitendo cha wamiliki kuanza kuwafukuza madereva ni cha uonevu kwani walikuwa wanadai haki zao za msingi.
“Tutafuatilia kujua kama huyo dereva aliyefukuzwa aliajiriwa kwa mkataba na kama hakuwa nao sisi kama chama tunao uwezo wa kumshtaki mmiliki,” alisema Masanja.
SERIKALI YAONYA
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga, alisema Serikali itawachukulia hatua wamiliki wote watakaobainika kuwafukuza kazi madereva kutokana na mgomo huo.
“Sisi kama Serikali hatujapata taarifa kama kuna wamiliki wameanza kuwafukuza madereva wao lakini kama ikitokea dereva akafukuzwa aje na vielelezo sisi tutachukua hatua stahiki” alisema Dk. Mahanga.
Mei 4 madereva wa mabasi ya mikoani na nchi jirani pamoja na daladala walifanya mgomo kwa siku mbili wakishinikiza serikali kufuatilia madai yao ya kupatiwa mikataba bora ya ajira pamoja na kutorudi shule kusoma kila baada ya miaka mitatu.
DC MAKONDA
Serikali imetimiza masharti ya madereva kwa kuunda kamati ya kushughulikia kero na matatizo ya madereva ambayo inatarajia kuanza kazi yake Ijumaa.

Akizungumza Dar es Salaam jana,Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alisema kamati hiyo itakuwa ya kudumu ambayo itakuwa ikishughulikia kero na matatizo ya barabarani nchini.
Kamati hiyo itaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara Uchukuzi, Shabaan Mwinjaka na wajumbe wake ni Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Ajira, Katibu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wawakilishi watatu kutoka Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) na Kakoa.

Wengine ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na washiriki watano kutoka kwa chama cha madereva nchini.

Habari hii imeandikwa na Koku David, Veronica Romwald, Mauli Muyenjwa na Nora Damian, Dar es Salaam

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles