30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Otuck William kumwaga fursa kibao kwa mastaa Bongo

CHRISTOPHER MSEKENA

TASNIA ya burudani nchini imekua kubwa kiasi kwamba mastaa wanahitaji elimu ya kuwawezesha kunufaika na biashara wanazofanya ndani ya sanaa.


Unaweza kuona jinsi kampuni, taasisi na mashirika mbalimbali yakiwatumia wasanii kusogeza ajenda zao kwenye jamii kwa urahisi.


Otuck William ni miongoni mwa wasanii wachache wa Tanzania wanaofanya kazi zinazohusiana na muziki akishirikiana na mashirika ya Kimataifa huko amezioa fursa kibao kwa watu maarufu Bongo.


Akizungumza na Swaggaz wiki hii katika ofisi za gazeti hili, Otuck alisema: “ Nafanya shughuli zinazohusiana na muziki ila siyo muziki wa biashara, mimi huwa nafanya kazi na mashirika tofauti tofauti na taasisi lakini lengo langu kubwa ni kwenye masuala ya afya sababu nina historia ya kufanya ‘medicine’ (udaktari) ambayo nafanya mpaka sasa.”


Otuck anasema sanaa ina ushawishi mkubwa kwenye jamii ndiyo maana wadau mbalimbali wamekuwa wakiwatumia watu maarufu hasa wanamuziki kwenye kampeni zao ili kufikisha ujumbe kwa urahisi kwenye jamii.

Otuck na John Makini


“Kama unavyojua Wizara au shirika linaweza kufanya kampeni, wakachukua wasanii wakaenda kutumbuiza au wakatengeneza nyimbo pia kumekuwa na vitu vingi ambavyo mimi binafsi na wenzangu tumekuwa tukijifunza namna ambavyo wasanii wanahusishwa kwenye hizo kampeni,” anasema Otuck.
Otuck ambaye hivi anatamba na wimbo, Push It aliomshirikisha Joh Makini, anasema tayari amefanya kampeni nyingi zilizomkutanisha na mastaa wakubwa kama vile Yvonne Chaka Chaka hivyo ana uzoefu wa kuona wapi wasanii wakaosea na wapi wanapatia.


“ Baada ya kupata ujuzi huo mimi na rafiki zangu wanaokaa Marekani, TrevMoMatic na dada Elizabeth anayetokea Chuo Kikuu Chicago tumegundua tunaweza kusaidia kwa namna fulani. Sisi tunaweza kufika pande zote mbili, tunaweza kufikia upande wa wasanii na tunawafikia wale wapangaji wa hizo kampeni.


“Sasa ni namna gani tunaweza kutengeneza urahisi utakaowasaidia wasanii na kazi wanazofanya kwenye hizo kampeni ziwe na matunda zaidi kuliko inavyofanyika sasa. Wasanii wengi wanapenda kufanya kampeni za kujitolea ila hawajui wanaanzia wapi, hawana ujuzi wa kutosha na hawa wanaowaita wanajua udhaifu wa wasanii wanawasainisha mikataba ambayo inawaumiza.


“Wapangaji wa kampeni wengi wao hawawajui wasanii, hawajui thamani ya wasanii na vitu vingine vingi kwahiyo tunatarajia kutengeneza ‘platform’ ambayo itakuwa na uwezo wa kuunganisha pande zote hizi mbili kwa wakati mmoja, huo ni mradi ambao tumepanga kuanza kuufanya mwakani.”


Aidha, Otuck anasema washirika wao wakubwa kwenye jukwaa hilo ni watu wa Marekani na itaanzia Tanzania ikifanikiwa itakwenda kwenye nchi zingine za Afrika sababu kuna nafasi kwa mastaa ndani ya mashirika kama vile Umoja wa Mataifa, Unicef na mengineo lakini wasanii hawana uwezo wa kuzifikia fursa hizo.


Otuck anasema jukwaa hilo ambalo jina bado limewekwa kapuni litatambulishwa mwakani na sasa bado wanaendelea kufanya mazungumzo na wafadhili ili waweze kudhamini mpango huo utakaotoa fursa kwa mastaa wa Bongo.


“Tukikamilisha mpango huu tutakutana na wasanii na wale watakaokuwa tayari tutawapa mafunzo na tutatengeneza kampeni yetu wenyewe kuonyesha jinsi kampeni zinavyoweza kufanyika tofauti na ilivyozoeleka pia tutawangunisha wasanii na taasisi zinazohitaji kufanya nao kazi,” anasema.


Hali kadhalika, Otuch ambaye ni bosi wa taasisi za Young and Alive Tz na Tayarh Coalition na balozi wa Sdsn Youth anasema: “ Kumekuwa na jitihada nyingi za kuhakikisha wasanii au watu maarufu kujihusiaha kwenye kampeni za kijamii.


“Mara nyingi watu wanaona kampeni zinazotengenezwa na Wizara ya Afya na washirika wa maendeleo kama Unicef na wengine hasa kwenye afya lakini mara nyingi tatizo linakuwa wasanii wanaohusishwa hawahusishwi toka mwanzo wa utengenezaji wa hizo program, wenyewe wanakuja kuhusishwa mwishoni kitu ambacho hakitengenezi matokeo makubwa kwa msanii.


Kwahiyo lengo la hii programu ni kuhakikisha wasanii wanatumika vizuri vile ambavyo wao wanataka na wanafaidika lakini pia matokeo ya kushirikishwa kwao yanakuwa makubwa.”
Katika upande wa muziki, mkali huyo wa RnB nchini anasema mwakani ataachia albamu yake itakayokuwa na sehemu mbili ya Bongo Fleva na RnB ili kuwapa ladha tofauti mashabiki.

“Muziki umehamia mtandaoni ni watu wachache wanaotumia CD sababu tayari kuna ‘platforms’ za kupakua na kusikiliza muziki tofauti za zamani wasanii walikuwa wanaogopa kutoa albamu wakihofia kupata hasara kwahiyo mashabiki waisubiri albamu yangu itatoka mwakani,” anasema Otuck.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles