31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Shibuda atoa neno ripoti uchaguzi Serikali za Mitaa

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, John Shibuda amesema kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa ni fursa ya kujenga mwamko mpya wa kusahihisha makosa ili yasiendelee kutokea kwenye chaguzi zijazo.

Shibuda ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Chama cha Ada Tadea, ameyasema hayo katika taarifa yake wakati akipokea taarifa ya ripoti ya uangalizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji  iliyofanywa na asasi ya kirai ya Tafeyoco.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Novemba 24, 2019 vyama vya upinzani vya Chadema, CUF, ACT- Wazalendo, UPDP na Chaumma vilisusia kushiriki kutokana na kile walichodai kutoridhishwa na mwenendo mzima wa uchaguzi huo huku vyama vya NRA, DP, AAFP na TLP vikishiriki.

Miongoni mwa mambo yaliyojitokeza katika mchakato ni asilimia kubwa ya wagombea wa vyama vya upinzani kuenguliwa baada ya kukosa sifa huku baadhi ya waliochukua fomu wakijikuta wakishindwa kurudisha baada ya ofisi za Serikali kufungwa.

Akizungumza huku akitumia nahau na methali, Shibuda amesema kuwa ukweli uliopo taifa lina fadhaa ya mgogoro wa kuhusu kuwepo kwa kasoro ya uborongwaji na uparaganishwaji wa ndiyo na wa siyo kwa kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

“Kwa hiyo sasa, msemo wa hakuna chema kisicho na kasoro umetua vyema katika uchaguzi wa serikali za mtaa wa mwaka huu. Kwa kutambua kwamba leo kusema uchaguzi wa serikali za mitaa haukuwa na kasoro ni sawa na kujaribu kuficha kaa la moto kwenye mfuko wa kanzu.

“Kwa kutambua wadau wa vyama vya siasa na umma wa wakereketwa wa masuala haya wana fikra ya taftishi za kusaka suluhu, suluhu inayohitajika ni kujenga utulivu wa fikra kwa uwazaji wa kuelekea katika dira ya msimu wa duru za siasa za uchaguzi wa mwakani,” amesema Shibuda.

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Vyama vya Siasa, alipokea maoni ya Tafeyoco, ambapo amesema ni sehemu ya taarifa itakayoondoa ukomo na ulegevu kwa mambo ya mtu mwenye taarifa za kutaka kujua asiyoyajua.

“Msema kweli ni mpenzi wa Mungu sasa tukiri ndani ya jamii yetu kuna gumzo za kimya kimya na mijadala ya uwazi ya kuhusu fikra za kutangatanga za hoja ya kutaka kujua endapo kuna uongo au ukweli unaogusa changamoto za Serikali za mtaa,” amesema Shibuda.

Akiwasilisha ripoti ya uangalizi wa uchaguzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tafeyoco, Elvice Makumbo amesema miongoni mwa mambo waliyoyabaini ni baadhi ya vyama vya siasa kushinda kushirikiana na wagombea wa vyama.

Hata hivyo alipongeza vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo na kusema kuwa sasa ni vema Serikali irekebishe kasoro zilizojitokeza ili sisijirudie wakati mwingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles