NA SWAGGAZ RIPOTA
GUMZO kubwa kwenye kiwanda cha burudani wiki hii ni ile taarifa kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuzifungia nyimbo 13 za wasanii wa Bongo Fleva kwa madai ya kukosa maadili ya kimaudhui yaliyo kinyume na kanuni za huduma ya Utangazaji (2005) na kuvitaka vyombo vya habari yaani redio na runinga kuacha mara moja kuzicheza kuanzia Februari 28 mwaka huu.
Nyimbo hizo zilizofungiwa zilipelekwa TCRA na Baraza la Sanaa na Taifa (BASATA ni Waka Waka na Hallelujah za Diamond Platnumz, Pale Kati Patamu, Makuzi, Mikono Juu za Ney wa Mitego , Chura, Nimevurugwa za Snura, Nampaga wa Barnaba, Nampa Papa wa Gigy Money, Uzuri Wako wa Jux, Hainaga Ushemeji wa Man Fongo, I Am Sorry JK wa Nikki Mbishi, Kibamia wa Rostam pamoja na Tema Mate Tuwachape wa Madee.
Tukio hilo liliongozana na lingine kubwa la kufungiwa miezi 6 kwa msanii Ibrahim Mussa ‘Roma Mkatoriki’ baada ya kukaidi wito wa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza aliyemwita ofisini kwake ili wazungumze namna ya kuyabadili maudhui ya wimbo wa Kibamia huku Ney wa Mitego akipewa onyo na kuelekezwa kuurekebisha wimbo wake mpya, Mikono Juu.
Matukio hayo yamezua gumzo kwenye sekta ya burudani huku wadau, mashabiki na wasanii mbalimbali wakitoa mitazamo yao juu ya hatua za kuzifungia nyimbo hizo.
HOJA ZAIBUKA
Wimbo kama Uzuri Wako wa Jux ulitoka Septemba 2013, Tema Mate Tuwachape wa Madee uliotoka mwaka 2014, Pale Kati Patamu wa Ney wa Mitego na Hainaga Ushemeji ya Man Fongo zilitoka mwaka 2016, kwa kifupi ni nyimbo za kitambo sana.
Hazipo kwenye mzunguko, zimeshachuja, wasanii wake walishatoa kazi zingine mpya. Zimebaki historia kwenye mtandaoni kama YouTube nk, kwa hiyo kitendo cha kuzifungia sasa hivi hakimpi hasara yoyote msanii japo kuwa kama kuna madhara basi tayari jamii imeathirika.
Kwanini nyimbo zisizo na maaadili zisifungiwe punde zinapotoka au kabla hazijatoka ili kuepusha madhara kwenye jamii? Nasikia kuna kitengo cha maudhui, kinafanya kazi gani kama nyimbo zinakwenda redioni, runinga na kwenye tovuti mbalimbali kisha baada ya miaka kadhaa ndiyo zinafungiwa.
GIGY MONEY AONGEA
Swaggaz lilifanya mazungumzo na msanii Gigy Money ambaye wimbo wake Nampa Papa umefungiwa naye akasema: “ Mimi naona fresh tu, kwa sababu sijafungiwa peke yangu lakini pia ni wimbo wa zamani, sasa hivi nipo bize ‘na-push’ wimbo wangu mpya, Mimina,” anasema.
MAADILI YAPI YAFUATWE?
Tunaishi katika ulimwengu wa utandawazi na sisi kama watanzania tuna maadili yetu ambayo kwa gharama yoyote ile ni lazima tuyalinde tusikubali kuyapoteza, ila ni maadili gani hayo?.
Tukumbuke kuwa katika dunia ya leo huwezi kuzuia wasanii wasitoe nyimbo zinazoendana na soko la dunia. Dunia ndiyo inataka twende huko ambapo nyimbo nyingi kikwetu kwetu zipo kinyume na maadili.
TUFANYE NINI?
Kwa taratibu zifuatazo tutaweza kulinda maadili huku tukishindana kwenye soko la dunia la muziki lililojaa nyimbo zenye maudhui ambayo yangefanywa na msanii wa kitanzania basi angefungiwa mara moja.
Kamati ya maadili BASATA na TCRA wanapaswa kupokea na kusikiliza nyimbo za wasanii kabla hazijatoka na kuziweka katika madaraja matatu yafuatayo.
PRIVATE AUDIENCE
Hawa ni wasikilizaji au watazamaji binafsi wanaoweza kusikiliza au kutazama kazi za sanaa zenye maudhui ya faragha katika klabu za usiku, kasino nk.
Muziki au filamu zinazowaburudisha mashabiki hawa (Private Audience) haziwezi kupigwa redioni au kwenye runinga, hivyo mtu kwa mapenzi yake akitaka kutazama au kusikiliza kazi hizo aende huko kwenye klabu za usiku.
PUBLIC AUDIENCE
Hawa ni watazamaji au wasikilizaji wenye itikadi moja. Nyimbo au video wanazotazama ni zile zinazohusu jamii yao tu. Mfano kukiwa na mkutano wa chama fulani cha siasa watatumia nyimbo au video zenye jumbe za kusifu chama au Ilani zao.
Nyimbo hizo haziwezi kupigwa kwenye redio au runinga na kusikilizwa na watu wote. Hutumika na watu wenye itikadi moja wanapokutana. Mfano nyimbo maarufu za kampeni haziwezi kuingia kwenye mzunguko (Mainstream) na kusikilizwa nchi nzima sababu kuna watu wenye itikali na mitazamo tofauti.
MASS AUDIENCE
Hizi ni nyimbo ambazo hazina madhara kwa jamii yote. Watoto kwa wakubwa wanaweza kusikiliza na kuburudika, hazina mipaka.
USHAURI MUHIMU
Hivyo kabla nyimbo hazijatoka, kamati inayohusika na maudhui inapaswa kusikiliza kazi za wasanii wake na kuzipa madaraja hayo ili kuepusha ‘fungia fungia’ au madhara ya kubomoa maadili kwenye jamii.