ZAINAB IDDY na ADAM MKWEPU
-DAR ES SALAAM
KIUNGO mpya wa Simba, Haruna Niyonzima, ndiye mchezaji aliyekuwa na mvuto zaidi katika Tamasha la Simba ‘Simba Day’ lililoambatana na mchezo wa kirafiki baina ya timu hiyo na Rayon Sports ya Rwanda kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana.
Niyonzima alijiunga na Simba katika kipindi cha dirisha la usajili lililofungwa hivi karibuni akiwa mchezaji huru, baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga aliyoitumikia kwa misimu sita mfululizo.
Mchezaji huyo ambaye pia ni nahodha wa timu ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’, amekabidhiwa jezi namba nane iliyokuwa ikitumiwa na kiungo mwenzake, Mwinyi Kazimoto, ambaye kwa sasa anavaa jezi namba 24.
Niyonzima ambaye aliingia dimbani kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mohammed Ibrahim ‘Mo’ aliyefunga bao la ushindi la Simba, alianza kuwapagawisha mashabiki wa timu hiyo mara jina lake lilipotajwa wakati wa utambulisho wa wachezaji kabla ya mchezo.
Akifahamu jinsi alivyokuwa akisubiriwa kwa hamu na watu wa Simba, Niyonzima hakutaka kuremba zaidi ya kufanya kile kilichowavutia Wekundu wa Msimbazi hao kumsajili kwa kupiga pasi za maana, huku akiuchezea mpira kadiri alivyotaka kama ilivyo kawaida yake.
Kwa ujumla, Tamasha la Simba Day lilifana vilivyo, huku likichagizwa na ushindi huo wa bao 1-0, shujaa wa Wekundu wa Msimbazi hao jana akiwa ni Mo aliyecheka na nyavu za Rayon Sports dakika ya 15 kutokana na pasi ya Emmanuel Okwi.
Mchezo huo ulianza kwa kasi ambapo timu zote zilikuwa zikicheza kwa tahadhari, huku wakishambuliana kwa zamu.
Dakika ya 10, Okwi alikosa bao baada ya shuti lake kuokolewa na kipa wa Rayon, Evarist Mutuyimana, ikiwa ni kutokana na pasi ya Muzamiru Yassin.
Baada ya kosa kosa hiyo, Mo alizitikisa nyavu za wapinzani wao kutokana na shuti kali akiwa nje ya 18.
Dakika ya 21, mwamuzi alikataa bao la pili la Simba lililofungwa na Okwi baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Shiza Kichuya, ikidaiwa mfungaji aliupiga mpira ukiwa katika mikono ya kipa Mutuyimana.
Dakika ya 28, kipa wa Simba, Aishi Manula, aliokoa hatari katika lango la Simba baada ya kutokea piga ni kupige.
Simba ilikwenda mapumziko ikiwa kifua mbele kwa bao la Mo ambapo kipindi cha pili, Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, aliwaingiza Niyonzima, Jonas Mkude, Nicholous Gyan na Ally Shomari, kuchukua nafasi za Jamal Mwambeleko, Mo Ibrahim, James Kotei na Okwi.
Baada ya mabadiliko hayo, Simba iliongeza kasi ya kutafuta bao la pili kwa kulisakama lango la Rayon kwa dakika zaidi ya 10, huku washambuliaji wao, Gyan na John Bocco wakishindwa kutumia nafasi walizopata.
Dakika 56, Bocco alikosa bao la wazi baada ya kupokea pasi kutoka kwa Kichuya, ambapo shuti lake lilitoka pembeni kidogo ya lango la wapinzani wao.
Dakika ya 69, Simba ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Kichuya aliyeumia na nafasi yake kuchukuliwa na Mwinyi Kazimoto, kabla ya Said Ndemla kuingia dakika ya 75 kuchukua nafasi ya Mzamiru.
Dakika ya 73, Niyonzima almanusura aipatie Simba bao la pili baada ya kuwatoka mabeki wa Rayon, lakini shuti lake lilitoka nje kidogo ya lango.
Dakika ya 80, Rayon walikosa bao la kusawazisha baada ya kipa wa Simba, Manula kuokoa hatari iliyoelekezwa langoni mwake kutokana na mpira wa kona.
Dakika ya 85, almanusura Simba wapate bao lakini shuti la Niyonzima alilopiga, lilitua mikononi mwa kipa wa Rayon.
Kikosi cha Simba: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Jamal Mwambeleko/Ally Shomari dk56, Method Mwanjale, Salim Mbonde/ Bukaba, James Kotei/ Jonas Mkude, Shiza Kichuya/ Mwinyi Kazimato dk 69, Mzamiru Yassin, John Bocco/Laudit Mavugo dk83, Emmanuel Okwi/Nicholous Gyan dk 46 na Mohamed Ibrahim/ Haruna Niyonzima dk 46.
Rayon: Evarist Mutuyimana, Eric Rutanga, Gabriel Mugabo, Ally Niyonzima, Idrisa Nsengiyuma, Nova Bayama, Piere Kwizera, Alhassane Tamboura, Tidiane Kone na Gilbert Mugisha.