Na MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema nishati ya uhakika ya umeme itatokomeza umasikini nchini Tanzania ifikapo mwaka 2030.
Profesa Muhongo aliyasema hayo alipokuwa akizindua Jukwaa la Nishati Tanzania (TEP) pamoja na mkutano wa siku mbili kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu, jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo unaolenga kujadili upatikanaji wa nishati endelevu ya kutosha kwa bei nafuu ya uchumi wa viwanda Tanzania, unakutanisha wadau mbalimbali zikiwemo kampuni za utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi nchini kama vile Statoil, BG na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Wadau wengine ni pamoja na kampuni za kuzalisha umeme kama vile Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Songas pamoja na mabalozi wa nchi mbalimbali, taasisi za kifedha na viongozi wa Serikali.
Profesa Muhongo alisema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana itakayopelekea Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 kama Dira ya Maendeleo ya Taifa inavyofafanua.
Waziri Muhongo alisema nishati ya kutosha itapelekea uanzishwaji wa viwanda vidogo hususani katika maeneo ya vijijini na kuzalisha ajira hivyo kupunguza wimbi la vijana kuhamia mijini kutafuta maisha.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Florens Luoga, alisema kupitia Jukwaa la Nishati Tanzania linaloundwa na wataalamu kutoka Tanzania na Uholanzi, wanaangalia namna ya kushirikiana kupitia kubadilishana uzoefu kupitia programu mbalimbali.