26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

UDZUNGWA HIFADHI YA KIPEKEE ISIYOJULIKANA

Na LEONARD MANG’OHA


UWAPO wa maziwa makuu ya Viktoria, Tanganyika na Nyasa Mbuga ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Ngorongoro, Mikumi, vyura wa Kihansi na visiwa vya marashi ya karafuu ni miongoni mwa mambo yanayoitambulisha Tanzania kimataifa.

Tanzania imekuwa ni nchi yenye bahati ya kuwa na idadi kubwa ya vivutio vya utalii na vya kipekee, ikiwa pia na eneo lilipogunduliwa fuvu la binadamu wa kale zaidi huko Oldvai Gorge na hifadhi yenye idadi kubwa ya Sokwe za Gombe na Mahale mkoani Kigoma.

Idadi kubwa ya mbuga na hifadhi za wanyama, mali kale, milima mirefu mito na maeneo tengefu yanaifanya Tanzania kuendelea kuwa lulu si tu Afrika mashariki, ni bara lote la Afrika na duniani kote.

Safu ya milima ya Usambara, mlima Meru, chemuchemu ya maji moto na mchana unaotembea (steping stones), mapango ya Amboni na mengineyo vimeendelea kuifanya nchi kuwa maarufu na hata baadhi ya vivutio vyake kutajwa katika maajabu saba ya dunia.

Vivutio hivi vya kipekee ndiyo sababu kuu inayowasukuma watalii wengi kutoka mataifa mbalimbali duniani kuja hapa nchi kushuhudia utajiri wa maliasili ilizotunukiwa Tanzania.

Nimejaribu kutaja baadhi tu ya mambo na vivutio kuonesha namna ambavyo Tanzania imejaliwa na si jambo rahisi kutaja vyote kutokana na wingi wake.

Lengo kuu la makala haya si kuorodhesha mlolongo wa vivutio na maliasili zilizopo nchini, bali ni kuzungumzia moja ya vivutio vya utalii vyenye sifa za kipekee hapa nchini na zisizopotikana mahala pengine nchini na hata nje ya nchi. Si kingine bali ni Hifadhi mlima ya Udzungwa.

Udzungwa, ni hifadhi inayopatikana katika Wilaya ya Kilombero kiasi cha kilomita 60 kutoka ulipo Mji wa Mikumi, na sehemu kubwa ipo Iringa Vijijini mkoani Iringa.

Ukiwa unaelekea katika mlima huo, utashuhudia mandhari nzuri ya miti mirefu kwa mifupi na uoto wa asili wenye rangi ya kijani kibichi muda wote si kiangazi wala masika.

Kwa wale waliobahatika kupita eneo hili, wamepata kuona uwepo wa reli inayoelekea Zambia ikiwa imejengwa umbali wa mita zisizopungua 30 kutoka ilipo barabara.

Katika njia hiyo ndiko yanakopatikana maporomoko ya Mto Ruaha ambao pia umekuwa ukichangia katika kuzalisha umeme.

Unapoingia katika eneo la mapokezi ya hifadhi hii, unakutana na geti lililotengenezwa katika muundo wa pembe za tembo kando kukiwa na miti mingi na hali ya hewa ya eneo hii ni baridi.

Uwepo wa viumbe hai wasio mimea

Ni hifadhi pekee iliyo na jumla ya viumbe hai (species) wasio mimea aina 70 ikijumuisha vipepeo, mijusi, nyani, mbega, ndege na wengine wengi.

Kuna jumla ya aina 400 za vipepeo wakubwa na wadogo na kati ya vipepeo hao, aina tatu zinapatikana katika hifadhi hiyo tu na hawapatikani sehemu nyingine yoyote duniani.

Mbali na kuwapo kwa takribani aina 11 za nyani katika hifadhi hii, pia aina tano za nyani hao hazipatikani sehemu nyingine duniani zaidi ya Tanzania na kati ya hizo aina mbili hupatikana Udzungwa pekee.

Uwapo wa Mbega wekundu wanaofahamika kama ‘red collabus’ sanje Crested Mangabey’ aliyeguduliwa mwaka 1979, ni moja ya mambo yanayoifanya hifadhi hii kuwa ya kipekee duniani na kuwa katika kundi la vivutio muhimu vya utalii nchini.

Mbuga hii ina ukubwa wa mita za mraba 1990 ikihusisha Mkoa wa Iringa kwa asilimia 80 na 20 katika Mkoa wa Morogoro.

Maporomoko ya maji kutoka mlimani kwa kasi kubwa katika eneo lenye urefu wa mita 170 kwenda juu ni miongoni mwa yale yanayofurahisha wakati unapopanda mlima Udzungwa.

Pamoja na sifa lukuki za hifadhi ya mlima huu, bado haufahamiki kwa watalii wengi si tu wa nje hata wa ndani bado hawana ufahamu mkubwa wa kivutio hiki kutokana na uelimishaji mdogo.

Serikali kupitia mamlaka husika inapaswa kuvitangaza zaidi vivutio ili kuiwezesha sekta ya utalii kuchangia kiasi cha kutosha katika mapato ya Taifa na kuharakisha ukuaji wa uchumi.

Mwaka 2014, takwimu zilionyesha kuwa kulikuwa na watalii milioni moja tisini na tano elfu mia nane themanini na wanane waliotembelea vivutio mbalimbali nchini na jumla ya Sh bilioni 4.2 zilikusanywa.

Idadi hii ni ndogo ikilinganisha na wingi wa vivutio vilivyopo nchini ikilinganishwa na nchi kama Uturuki ambayo hupokea kati ya watalii milioni nne hadi sita kwa mwaka.

Baadhi ya vivutia hushindwa kufanya vizuri kutokana  kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa miundombinu rafiki kwa watalii kama vile barabara na hoteli za hadhi ya kimataifa,

Miundombinu katika sehemu nyingi zenye vivutio si ya kuridhisha sana ambapo barabara nyingi huwa ngumu kupitika haswa kipindi cha masika.

Kidogo kwa upande wa hoteli wafanyabiashara wameweza kuwekeza  kwa kujenga karibu maeneo yote ya utalii japo hoteli nyingi zinaonekana kuwalenga watalii wa kati na wadogo.

Licha ya kuwa na hoteli katika sehemu nyingi za utalii, bado kuna uhitaji wa hoteli za hadhi ya kimataifa ambazo zitakuwa na uwezo wa kupokea wageni wenye kipato kikubwa .

Je, Serikali inafurahishwa na hali hii au ni lini utalii utaipa nchi heshima inayostahili kwa kuchangia kiasi kinachoendana na uhalisia wa vivutio vyetu.

Devote Mdachi ni Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), anasema wameanza kuchukua jitihada za kina kuhakikisha wanatangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Anasema ili kuhakikisha wanafanikiwa katika hilo wamekuwa wakitumia majarida maalumu kutangaza ambapo wameanzisha jarida liitwalo ‘Hard venture tourism’ linalotangaza vivutio visivyofahamika kwa wengi ikiwamo mali kale na hulisambaza kwa watu mbalimbali ndani na nje ya nchi kila wanapokuwa kwenye mkutano.

Anadai kuwa wameamua kutumia tovuti na mitandao ya kijamii kutangaza vivutio kutokana na watu wengi kwa sasa kupenda kutumia mitandao hiyo.

“Tunakazania kukuza utalii wa ndani kwanza kuhakikisha wananchi wanafahamu mambo yanayopatikana katika vivutio hivyo, mtu akienda Serengeti apate nafasi ya kufahamu mengi zaidi ya wanyama ambao wengi wetu hufikiria pale anapoambiwa kwenda huko.

“Ili kuhakikisha Watanzania wanajua nini zaidi kinapatikana huko, tumepanga kutumia kipindi cha 360 katika msimu huu wa pasaka kwenda Ngorongoro na Serengeti ili kuonesha umma fahari ya mbuga hizo,” alisema Mdachi.

Anakiri kuwapo kwa changamoto ya miundombinu katika baadhi ya maeneo ya utalii, lakini anasema Wizara ya  Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wizara nyingine zitaboresha mazingira ili kuvutia watalii wengi.

Anasema katika mwaka wa fedha 2017/2018 watakamilisha mpango wa kuwa na mkakati wa kutangaza utalii wa ndani ambao haukuwapo awali.

Anashauri baadhi ya taasisi kama vile Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutenga muda wa kutangaza utalii na kuweka gharama nafuu za kupeleka watalii wa ndani katika maeneo ya utalii hususan wakati wa sikukuu na likizo za wanafunzi za Juni na Desemba.

“Tumekaa na wamiliki wa mabasi na kuwaomba watumie mabasi yao kutangaza utalii, sisi tunawaandalia video ya kuelezea yale yanayopatikana huko. Kwa mfano mtu anayesafiri kupitia Mikumi aone na kuelekezwa yale ambayo anaweza kuyapata hapo ikiwa ataamua kushuka hapo,” alisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles