KOKU DAVID-DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema itakuwa ikishirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na Serikali za mitaa ili kuweza kuwajua walipakodi wake.
Kwa kushirikiana na NIDA, mamlaka ya mapato itakuwa ikitumia vitambulisho vya Taifa ili kutoa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ambayo hutolewa bila malipo yoyote.
Aidha kwa upande wa Serikali ya Mtaa, TRA itakuwa ikishirikiana na Serikali ya mtaa kuweza kujua walipakodi waliopo katika maeneo husika ili kuweza kuwafikia na kuwapa elimu mbalimbali inayohusu kodi.
Kwa mujibu wa TRA, lengo la ushirika huo ni ili kuongeza walipakodi wapya watakaowezesha mapato ya Serikali kuongezeka.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, anasema TRA imeweka utaratibu wa kurahisisha upatikanaji wa TIN ambapo itakuwa ikishirikiana na NIDA ili kumwezesha mwombaji kuipata kwa urahisi.
Anasema hiyo ni moja ya mikakati mbalimba ambayo TRA imekuwa ikiibuni kwa lengo la kusaidia katika kuongeza walipakodi wapya pamoja na mapato.
Anasema mwombaji wa TIN atatakiwa kuwasilisha kitambulisho chake cha taifa katika ofisi za mamlaka ya mapato ili aweze kupata TIN kwa urahisi.
Anaongeza kuwa waombaji wa TIN ambao watakuwa hawana kitambulisho, wanaweza kwenda katika ofisi za NIDA ambako watapewa namba ambayo wataiwasilisha TRA kwa ajili ya kupewa TIN, huku taratibu za kupatiwa kitambulisho cha taifa zikiendelea.
Kayombo anasema mikakati mbalimbali ambayo mamlaka hiyo imejiwekea, imekuwa ikiisaidia katika kufanikisha lengo lake la ukusanyaji mapato.
Anasema katika mwaka wa fedha wa 2018/19, imewekewa lengo la kukusanya Sh trilioni 18.1 na kwamba hadi sasa imeshakusanya Sh trilioni 11.96 ambazo ni kipindi cha miezi tisa ya mwaka huo wa fedha.
Anasema makusanyo hayo ni kuanzia Julai 2018 hadi Machi 2019 na kwamba katika robo ya tatu ya mwaka huo wa fedha wa 2018/19, Januari walikusanya Sh trilioni 1.30, Februari walikusanya Sh trilioni 1.23 na Machi Sh trilioni 1.43.
Anasema katika makusanyo ya nusu mwaka wa fedha 2018/19 kuanzia Julai hadi Desemba 2018, TRA ilikusanya Sh trilioni 7.99 ambayo ukuaji wake katika makusanyo ya mwaka uliopita kwa kipindi kama hicho ulikuwa ni asilimia 2.01.
Anaongeza kuwa Julai 2018 walikusanya Sh trilioni 1.20, Agosti Sh trilioni 1.27, Septemba Sh trilioni 1.36, Oktoba Sh trilioni 1.29, Novemba Sh trilioni 1.21 na Desemba walikusanya Sh trilioni 1.63.
Anasema katika kuhakikisha mamlaka hiyo inafikia malengo iliyojiwekea, TRA itaendelea kutoa elimu mbalimbali kuhusu masuala ya kodi ili kuwahamasisha walipakodi kulipa kodi kwa hiyari kwa maendeleo ya nchi.
Anasema pia itaendelea kusajili walipakodi wapya katika mikoa, wilaya na vitongoji mbalimbali nchini.
Anasema kila mwenye kipato, sheria inamtaka kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi, hivyo wananchi wanatakiwa kuendelea kuwa wazalendo kwa kulipa kodi kwa hiyari bila shuruti.
Kayombo anasema wakwepa kodi hawana haki ya kuhoji maendeleo na kwamba ili wananchi wapate haki ya kuhoji maendeleo, wanatakiwa kulipa kodi kwanza kwa hiyari ili Serikali iweze kuwafanyia maendeleo katika maeneo mbalimbali.
Mantiki inadai kwamba asiyewajibika asipige kelele na kuwanyooshea kidole wenzake na kudai wote wawajibike kwani wana makosa makubwa kwani ulipaji kodi si hiyari ni lazima na wajibu na ni mtindo wa maisha ulimwenguni kote.