22.3 C
Dar es Salaam
Saturday, July 13, 2024

Contact us: [email protected]

Nguzo tatu za Magufuli

Na Mwandishi wetu-Dar es Salaam

IKIWA imebaki miezi minne Rais John Magufuli kufikisha miaka minne Ikulu na ukiwa umebaki mwaka mmoja, kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, akitarajiwa  kupeperusha tena bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa ajili ya kuongoza  awamu ya pili, miradi mitatu inayotarajiwa kuinua uchumi wa Tanzania imeonekana kuwa nguzo kwake.

Moja ya miradi hiyo ni ule alioweka jiwe la msingi  juzi ambao mwenyewe ameuita mboni ya Serikali, na yote inatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani.

Akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Rufiji (Stiegler’s Gorge) ambao kwa sasa umefikia asilimia 15 na unaotarajiwa kukamilika ndani ya miezi 35, alivitaka vyombo vya ulinzi kuuona kama mboni ya Serikali.

Rais Magufuli alisema mradi huo utakaogharimu Sh trilioni 6.5 unaotarajiwa kukamilika katikati ya mwaka 2022.

Mradi mwingine ambao unyeti wake unaonekana sawa na huo wa umeme ni wa kuboresha Shirika la Ndege la (ATCL)  ambapo Serikali imekuwa ikinunua ndege kwa fedha za ndani na kuzikodisha kwa shirika hilo.

Mradi wa  ujenzi wa Reli ya Kisasa ya (SGR), ambao pia unatumia fedha za ndani nao umo kwenye orodha hiyo hiyo .

Tofauti na miradi ya barabara na ile ya madaraja makubwa ambayo baadhi ilikuwa kwenye mipango mbalimbali ya Serikali, miradi hii mitatu imeanzishwa ndani ya uongozi wa Rais Magufuli na amekuwa akiitekeleza kwa fedha za ndani.

Yeye mwenyewe Rais Magufuli  amekuwa akieleza kuwa, kukamilika kwa miradi hiyo, kutafanya kasi ya maendeleo kuongezeka na watu wengi zaidi kupata ajira.

Katika uchaguzi mkuu ujao, Magufuli atakuwa akiomba ridhaa ya kuongoza kwa awamu ya pili huku akiwa ameifanya ATCL kuwa na takribani ndege 10 mpya.

Itakumbukwa  wakati akiingia madarakani Rais Magufuli alilikuta shirika hilo likiwa hoi kwa kila kitu zaidi  likiwa na ndege moja.

Pia atakuwa akiomba kuchaguliwa kuongoza awamu ya pili wakati ambapo, Watanzania watakuwa wameanza kupanda treni za kisasa za umeme.

Jambo hilo linatajwa kuwa ni historia kwa taifa kwani reli hiyo ni ya kwanza ya kisasa Afrika Mashariki na Kati.

Zaidi wakati akiomba kura, utekelezaji wa mradi wa umeme wa Rufiji utakuwa ukiendelea ikiwa ni kukamilisha ndoto ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, iliyokaa kwa zaidi ya miaka 40 tangu utafiti wa kwanza wa mradi huo ufanyike.

Mradi wa umeme

Mradi wa umeme wa maji wa Rufiji, unaotarajiwa kuzailisha Megawati 2,115, unatajwa kumaliza kabisa tatizo la umeme nchini na kupunguza gharama ya nishati hiyo jambo litakalochochea maendeleo ya viwanda.

Kutokana na uwekezaji huo, uzalishaji wa umeme nchini utaongezeka zaidi kutoka uzalishaji wa sasa wa megawati 1,560.

Mpango wa Serikali ni kufikia uzalishaji wa umeme wa megawati 5,000 mwaka 2020 na hatimaye megawati 10,000 mwaka 2025.

Rais Magufuli akiweka jiwe la msingi kwenye mradi huo juzi alisema kukamilika kwake kuna manufaa si tu kwenye nishati bali pia kwenye sekta nyingine za uchumi na uzalishaji.

“Ndugu zangu mradi huu utatufanya tuwe na umeme wa kutosha na wa uhakika, utakaa kwa zaidi ya miaka 60 na bei yake itakuwa chini na kwa tathimini tuliyoifanya vyanzo vingine vingetugharimu.

“Manufaa mengine; kama nilivyogusia mradi huu utakuwa kichocheo kikubwa kwa maendeleo ya sekta ya viwanda, azma hii haiwezi kufikiwa bila kuwa na umeme wa uhakika na wa bei nafuu, ni dhahiri kulingana na bei ya umeme kwa sasa baadhi ya wajasiriamali wanashindwa kuanzisha viwanda” alisema.

Naye Waziri wa Nishati Dk. Medard Kalemani alisema, “tutazalisha kilovoti 400, ni umeme mkubwa utakaoweza kutumika viwandani utakaosafirishwa kwenda Chalinze hadi Dar es Salaam na mwingine hadi Dodoma na ndiyo umeme utakaotumika pia katika treni ya mwendokasi.

“Rais Magufuli ulitoa maelekezo kwamba lazima tupate megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025 mradi huu ni kichocheo kikubwa sana kuelekea kupata megawati hizo, utatosha kuendesha shughuli za viwanda,” alisema.

Mradi huu ambao Rais Magufuli alisema ukikamilika uitwe Nyerere, ukikamilika utakuwa mkubwa kuliko yote Afrika Mashariki.

Bwawa linalofuata kwa kuzalisha umeme mwingi ni lile linalojengwa Bujagari nchini Uganda, likitarajiwa kuzalisha megawati 300.

Bwawa kubwa zaidi lipo Ethiopia ambalo linalendelea kujengwa likikamilika litazalisha megawati 6,450 na ujenzi wake utakamilika 2022.

La pili lipo Mambira Nigeria linazalisha megawati 3,050, la tatu liko Ethiopia ambalo ni Shaika likizalisha megawati 2,160. na la nne ndo linalojengwa nchini.

Ameuita nradi wa kufua umeme wa Rufiji utakaogharimu Sh trilioni 6.5 kuwa ni mboni ya Serikali, utakapokamilika unatarajiwa kuongeza umeme unaozalishwa kutoka megawati 1, 500 hadi 5, 000 mwaka 2020.

Shirika la ndege

Moboresho yaliyofanywa na Rais Magufuli ndani ya miaka mitatu ATCL  lililoanzishwa mwaka 1977, yamefanya sasa abiria wake kuongezeka kwa zaidi ya mara tano.

Januari 11, Rais Magufuli akipokea ndege mpya ya sita aina ya Airbus A220-300, ambayo sasa imefanya ATCL kuwa na ndege tisa, alisema bado nyingine zaidi zitakuja.

Katika hafla hiyo, Rais Magufuli aliagiza ndege za Serikali zilizokuwa zikibeba viongozi, Fokker 28 na Fokker 50 zipakwe rangi na zibebe abiria.

Pia kabla ya maboresho ya shirika hilo yaliyofanywa na Rais Magufuli, shirika hilo lilikuwa na ndege moja aina ya Bombardier DASH8 Q300 iliyokuwa ikitumika tangu 2011.

Rais alisema ndege hiyo ya sita si ya mwisho, kwa sababu baada ya ile Dream Liner inayobeba watu 262 iliyowasili nchini mwaka 2018, itakuja nyingine ya aina hiyo ikiwa na uwezo wa kubeba watu 262 mwishoni mwa mwaka huu.

“Kwa hiyo Dream Liner zitakuwa mbili, Air Bus zitakuwa mbili, pia tumenunua ndege nyingine Bombardier, ili ziwe nne nayo italetwa mwishoni mwa mwaka huu au mwanzoni mwa mwaka ujao. Hivyo tutakuwa na ndege nane (mpya),” alisema.

Julai, 2018 akipokea Dreamliner, alisema “ndege zote hizi tumenunua kwa fedha zetu wenyewe, hatujakopa kwa mtu. Ndege hizi ni matokeo ya Watanzania kulipa kodi na kuchapakazi,”.

Rais Magufuli alisema “Shirika letu la ndege lilikuwa na hali mbaya sana, lilikuwa na ndege moja tu tena ilikuwa inafanyiwa matengenezo mara kwa mara, soko la ATCL lilishuka sana hadi kufikia asilimia 2.5,”.

“Tumeleta ndege hizi ili ziimarishe na kuongeza mapato yetu ya utalii nchini. Asilimia 70 ya watalii wanatumia ndege. Tunaboresha usafiri wa reli, majini na barabara. Waliodhani kuwa maboresho ya bandari hayana tija sasa wameaibika,”alisema.

Abiria waongezeka mara tano

Akiwasilisha bungeni hotuba ya hali ya uchumi kwa mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2019/20, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango alisema idadi ya abiria wa  ATCL imeongezeka kutoka 49,854 mwaka 2015/16 hadi 242,668 mwaka 2018/19.

Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 79.45 ya idadi ya abiria waliosafiri mwaka 2015/2016.

Alisema ongezeko la abiria wa ATCL linatokana juhudi za Serikali kuliboresha shirika hilo na kuliongezea uwezo wake wa kufanya kazi na kuwafikia watu wengi ndani na nje ya nchi kwa huduma bora za ndege.

Katika bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mwaka 2019/20, ATCL imetengewa Sh bilioni 500, zitakazotumika kukamilisha malipo ya ndege ya pili aina ya Dreamliner na Bombardier Q400 nne na injini moja ya akiba ya Bombardier.

Pia, itawezeshwa kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa ndege mbili aina ya A220-300.

Hadi 2020 ATCL itakuwa na ndege 10 mpya kutoka moja iliyokuwa nayo 2015. Idadi ya abiria imeongezeka kutoka 49, 854 mwaka 2015/16 hadi 242, 668 mwaka 2018/ 19.

SGR

Mradi ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ambao Aprili 2017, Rais Magufuli aliweka jiwe la msingi, awamu ya kwanza ya ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu wa kilomita 300 nao unabeba umuhimu mkubwa katika serikali ya Rais Magufuli.

Reli hii itajengwa kwa awamu tano ya kwanza ikiwa ni kutoka Dar-Morogoro, Morogoro –Makutupora, Makutupora-Tabora, Tabora-Isaka na Isaka -Mwanza na baadaye kwenda Congo, Rwanda na Burundi.

Ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam Morogoro utakaogharimu Sh trilioni 2.7 na kile cha Morogoro – Makutupora chenye kilomita 422 kitakachogharimu(Sh trilioni 4.4,  umeanza.

Mara kadhaa, Rais Magufuli amekuwa akisema mradi huu utagharamiwa kwa fedha za ndani, akisema utasaidia kuongeza kasi ya maendeleo ya nchi.

Ni reli hii inatajwa kuwa ya kwanza Afrika Mashariki na kati itakayokuwa na uwezo wa kupitisha treni zitakazoendeshwa kwa  umeme.

Itakuwa na uwezo wa kubeba treni yenye kuvuta mabehewa 100 na kubeba mzigo wa hadi tani 10,000 kwa mkupuo sawa na uwezo wa malori 500 ya mizigo.

Kulingana na mpango kazi, mradi wa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora , unatazamiwa uwe umekamilika Februari 2021.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, anasema kipande cha kwanza kati ya Dar es Salaam na Morogoro kilichoanza kujengwa Mei 2, 2017, kitakamilika Novemba 2019.

Mradi huu upo kwenye vipaumbele vilivyoainishwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mwaka 2019/20.

Bajeti ya wizara hiyo ni Sh trilioni 4.96 kwa mwaka wa 2019/20, ambapo kati yake Sh trilioni 3.62 ambazo ni takriban robo tatu ya bajeti ya wizara nzima, zimeelekezwa kwenye sekta ya uchukuzi ambako asilimia 75 zitatumika kujenga SGR na kuboresha miundombinu yake.

Bajeti hiyo, itatumika kukamilisha ujenzi wa reli kutoka Dar hadi Morogoro na kuweka miundombinu ya umeme na kuendeleza ujenzi huo kutoka Morogoro hadi Makutupora .

Kufikia 2020, kipande cha SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kitakuwa kimekamilika, mradi unatumia fedha za ndani, katika bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa 2019/20 umechukuaa Sh trilioni 3.62 ambayo ni asilimia 75 ya bajeti nzima.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles