Mwandishi Wetu
SIKU chache tangu wabunge wa upinzani watoke nje ya Ukumbi wa Bunge baada ya Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, kukataa hoja ya Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe, aliyetaka suala la kukamatwa wabunge lijadiliwe, Spika Job Ndugai, amewajia juu wanaokamata watunga sheria hao akisema hali hiyo itavuruga nchi.
Msimamo wa Ndugai umekuja wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akimtaka Freeman Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam jana ili ahojiwe kuhusiana na tuhuma za biashara ya dawa za kulevya.
Akizungumza bungeni jana muda mfupi kabla ya kuimbwa kwa wimbo wa Taifa ili Bunge liahirishwe, Ndugai, alisema: “Wakati wa mkutano huu palijitokeza baadhi ya wenzetu wakawa wanasema hadhi ya Bunge hili la 11 imeshuka, nataka kuwahakikishieni kwa Bunge hili la 11, hadhi yake iko palepale kama sio imepanda zaidi, mhimili huu hauna ugomvi wowote na Serikali, wala hatuna ugomvi wowote na mahakama wala hatufikirihi kuwa na hali ya namna hiyo.
“Mambo haya ya ofisa mmoja hapa na pale kusahau mipaka ya kazi zao na kuvuka kidogo ni mambo ya kawaida, mahali panapohusika watachukua hatua za kuweka sawasawa tu, haya ni mambo ya kujisahau sahau hivi, maana mimi naweza nikawa nawahitaji wabunge hapa kuna mambo tunatakiwa tufanye ambayo ni ya kitaifa, nimewaita wabunge mko hapa labda mko kwenye kamati, tunahitaji akidi, akikosekana mbunge mmoja inawezekana jambo hilo kwenye kamati lisipite.
“Kwa hiyo kama kuna junior officer (ofisa mdogo) huko anahitaji mbunge lazima aniambie, hatuwezi kwenda hivyo, kwa hakika tukienda tu kibabe kibabe namna hii, tutavuruga nchi haiwezekani, hatuwezi tukaenda hivi,” alisema Ndugai huku akipigiwa makofi na wabunge.
Februari 7, mwaka huu, Zitto, aliwasilisha taarifa bungeni akihoji sababu za Jeshi la Polisi kuwakamata wabunge wa upinzani bila sababu za msingi.
“Bunge letu liko katika nchi za Jumuiya ya Madola na linaongozwa na Katiba, kanuni, sheria za mabunge mengine, uamuzi wa maspika wengine na sheria zingine.
“Hivi karibuni, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), alikamatwa nje ya Bunge baada ya kuhudhuria vikao vya Bunge na hadi sasa Bunge halina taarifa.
“Kwa mujibu wa kanuni zetu na nchi za Jumuiya ya Madola, polisi wanapotaka kumkamata mbunge, lazima kwanza wampe taarifa Spika wa Bunge na baadaye Spika aliambie Bunge juu ya taarifa hiyo na kueleza ni kwanini mbunge amekamatwa.
“Pamoja na Lema kuwekwa ndani, Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali amefungwa jela miezi sita na hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kwa Spika wa Bunge na hata Bunge halijaelezwa juu ya tukio hilo.
“Katika hayo, Sheria ya Bunge ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge inakiukwa kwa sababu hata jana (juzi), Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alikamatwa bila Spika kuwa na taarifa.
“Mimi binafsi nilimpigia simu spika kumuuliza juu ya tukio hilo, spika akasema hakuwa na taarifa, hii ni dharau kubwa kwa Bunge.
“Mheshimiwa Naibu Spika, mhimili wa Bunge umedharauliwa mno kwani hata mimi nimepata taarifa, kwamba polisi wananisubiri ili nikitoka nje, wanikamate na siogopi kukamatwa.
“Kwa hiyo, naomba jambo hili lijadiliwe na litolewe uamuzi kwa sababu mwaka 2011, Bunge la Uingereza ililetwa hoja kama hii na Bunge likaijadili na kuitolea uamuzi,” alisema Zitto huku akitoa mfano wa wabunge waliowahi kukamatwa na polisi akiwamo Mbunge wa Nzega Vijijini, Dk. Hamis Kigwangalla (CCM).
Akitoa ufafanuzi wa taarifa hiyo, Dk. Tulia, alivitaja vifungu vya 6, 7, 8, 12 na 13 vya Kanuni ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, vinavyoeleza juu ya mbunge kukamatwa.
“Kwa hiyo, kifungu cha 12 kinasema Spika atapewa taarifa pale tu mbunge atakapokuwa akitakiwa kukamatwa kwa makosa ya madai na sio kwa makosa yasiyokuwa ya madai.
“Hivyo basi, taarifa ya mheshimiwa Zitto siwezi kuruhusu ijadiliwe kwa sababu makosa hayo siyo ya madai,” alisema Dk. Tulia.