23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

MANJI, GWAJIMA GIZANI

NORA DAMIAN Na AZIZA MASOUD

-DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, jana lilikwenda kufanya upekuzi ofisini kwa mfanyabiashara maarufu, Yusuph Manji, baada ya kufanya zoezi kama hilo juzi nyumbani kwake.

Manji pamoja na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, juzi waliripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam ikiwa ni wito wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye aliwataja katika orodha ya watu 65 wanaojihusisha na dawa za kulevya.

Hii ni mara ya pili polisi kufanya zoezi la upekuzi kwa Manji ambapo kwa mara ya kwanza walifanya zoezi hilo juzi nyumbani kwake pamoja na kwa askofu huyo.

Taarifa toka ndani ya Jeshi la Polisi zinadai kuwa Manji alitoka kituoni hapo akiwa ameongozana na maofisa kadhaa wa polisi na msafara wao kuelekea moja kwa moja zilipo ofisi zake.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, kuthibitisha taarifa hizo alijibu kwa kifupi: “Nipo kikaoni nipigie baadaye.”

Mwandishi alimpigia tena saa 1:00 usiku na alipoulizwa juu ya taarifa za mfanyabiashara huyo kuondolewa kituoni hapo, maongezi yalikuwa kama ifuatavyo:-

Mwandishi: Tumepata taarifa kuwa Manji ameondolewa hapo Central akiwa na polisi.

Kamanda Sirro: Ameenda wapi?

Mwandishi: Kuna taarifa kwamba ameenda kupekuliwa ofisini kwake na maofisa wa polisi.

Kamanda Sirro: Mimi sijui bwana.

Baada ya kutoa jibu hilo alikata simu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mchana, Sirro alikiri kuendelea kuwashikilia kituoni hapo, Manji na Gwajima.

Hata hivyo, jana Sirro hakuwa tayari kueleza walikokuwa wamewapeleka Manji na Gwajima juzi baada ya kuonekana wakiondoka kituoni hapo chini ya ulinzi mkali.

Wakati Sirro akikataa kuweka wazi hilo, taarifa ambazo gazeti hili limezipata toka kwa watu wa karibu na Manji na Gwajima, zinaeleza kuwa walielekea kwenda kufanya upekuzi majumbani mwao.

“Katika yale majina 65 Manji na Gwajima waliripoti jana (juzi) na upelelezi uliendelea mpaka usiku, walilala na hadi sasa wako mahabusu upelelezi unaendelea kufanyika.

“Kuna vitu ambavyo vinaashiria tuendelee kupeleleza, baada ya hapo wanaweza kufikishwa mahakamani au wasifikishwe…ni mapema mno kusema,” alisema Sirro.

Katika hatua nyingine, Sirro alisema pia wanawashikilia watu 11 baada ya kukamatwa wakiwa na kete 38 zinazodhaniwa kuwa ni za dawa za kulevya.

Pia alisema katika operesheni hiyo wamekamata magunia sita ya bangi.

 

Walioripoti jana

Hadi MTANZANIA Jumamosi linaondoka kituoni hapo majira ya mchana jana, waliokuwa wameripoti ni Mbunge Mstaafu wa Kinondoni, Idd Azzan na mmoja wa wamiliki wa Casino iliyoko ndani ya Hoteli ya Sea Cliff.

Azzan aliwasili kituoni hapo saa 3:06 asubuhi kwa gari aina ya Jeep yenye rangi nyekundu huku pia akiwa ameongozana na watu wengine wawili.

Saa 4:27 asubuhi mmoja wa wamiliki wa Casino iliyoko ndani ya Hoteli ya Sea Cliff aliwasili kituoni hapo akiwa kwenye gari aina ya Toyota Alifat yenye namba T 356 DHU.  

Mtu huyo ambaye alionekana kuwa na mwili mkubwa na umri uliokwenda kidogo, alishuka kwenye gari huku akisaidiwa na watu wengine wawili na baada ya hapo mmoja wa wasaidizi wake alizunguka katika buti ya gari na kuchukua kiti maalumu cha kukalia na kuingia nacho ndani ya kituo cha polisi.

Hata hivyo, idadi ya watu waliofika kituoni hapo kuhojiwa ni wanne tu kati ya 65 waliotajwa na Makonda.

 “Waliotajwa waje timu ya upelelezi inawasubiri wahojiwe na wanaoonekana wanahusika tutaendelea nao na wasiohusika tutawaachia.

“Hakuna sababu ya kuwa na woga wowote kwa sababu watu wanapiga simu sana na wengine wanatuma ndugu zao waje kuniona, kama umetajwa na unajua uko clean (msafi) huna tatizo lolote njoo watakuhoji wakiona huhusiki watakuachia,” alisema Sirro.

Alisema timu ya upelelezi iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa inayohusisha vyombo vya dola na vingine ina lengo la kuhakikisha kwamba upelelezi unakuwa wa haki kwa wanaotuhumiwa.

“Mpaka sasa waliofika ambao nimewaona wako wanne na wengine wanaendelea kuja lakini sitaweza kutaja majina yao. Anayefika si lazima akae ndani tukikuhoji tukafuatilia baadhi ya mambo ya msingi (Preliminary investigation) tunaweza kujua tuna mtu wa aina gani na tutajua kama unabaki au unatoka.

“Kama kuna vitu ambavyo vitatuonyesha kwamba kuna dalili fulani tutabaki na wewe kwa lengo la kutaka kuthibitisha ukweli wa yale ambayo upelelezi unakuwa umeonyesha,” alisema Sirro.

Alisema wako baadhi ya watu walioshindwa kuripoti na mawakili wao wametoa taarifa, lakini hakuwa tayari kutaja idadi wala majina ya watu hao.

Hali ilivyokuwa

Idadi ya watu nje ya kituo hicho cha polisi jana iliongezeka tofauti na siku zilizopita. 

Wingi huo ulimlazimisha Kamanda Sirro kuingilia kati na kutishia kuwatawanya kwa kutumia mabomu ya machozi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles