Na GRACE SHITUNDU
CHAMA cha NCCR Mageuzi, kimekuja na masharti mapya kwa chama chochote ambacho kitahitaji kushirikina nacho katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika oktoba mwaka huu.
NCCR Mageuzi ni miongoni mwa vyama vinne vilivyokuwa vimeungana katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2015 wakiwa chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Umoja huo uliundwa na vyama vya NCCR Mageuzi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF) na NLD na kumsimamisha Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, kuwa mgombea wao wa urais huku wakigawana majimbo na kata.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu maazimio yaliyofikiwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya NCCR Mageuzi, Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia, alisema katika uchaguzi mkuu ujao ushirikiano watakaoukubali ni ule utaokuwa na tija kwao.
“Nikiri kwamba katika ushirikiano uliokuwepo katika uchaguzi uliopita hatukuwa na mkataba wa kisheria ambao ulikuwa unaeleza maslai ya pande zote baada ya uchaguzi.
“Katika uchaguzi huu NCCR Mageuzi tupo tayari kushirikiana na chama chochote kwa kuzingatia maslai mapana ya nchi katika mchakato wote wa kushiriki Uchaguzi Mkuu lakini pia yawe na tija na kwetu pia,” alisema Mbatia.
Alisema katika uchaguzi uliopita wao walishirikiana na vyama vingine na kumuunga mkono wagombea waliosimamishwa na chama kingine hivyo endapo kuna chama kitahitaji ushiriakiano kwa mwaka huu, nao wawe tayari kuwaunga mkono wagombea wetu.
Alisema miongoni mwa madhumuni 18 ya NCCR Mageuzi ni kutwaa hatamu za dola na kujenga jamii yenye demokrasia na maendeleo.
“Ili tuweze kutekeleza dhumuni hili kwa vitendo chama chetu, tutashiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka mwaka huu kwa kusimamisha wagombea katika nafasi za udiwani, uwakilishi, ubunge, urais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibara na wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”alisema Mbatia.
Akizungumzia maazimio mengine waliyofikia katika Halmashauri Kuu ni pamoja na kutumia mfuo wa ndani ya chama kuhakikisha wanahamasisha na kuwashawishi wananchi kujiunga na chama hicho pia kushiriki katika kugombea nafasi mbalimbali.
“Pia viongozi wa chama katika ngazi mbalimbali wawahamasishe na kuwatia moyo wapiga kura ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao.
“Kupiga kura ni hatua mojawapo ya kimaendeleo yenye kuheshimu kazi iliyofanywa na waasisi wa taifa letu ya kupata haki ya kupiga kura na kupigiwa kura,” alisema Mbatia.
Alisema pia halmashauri kuu ya chama hicho imeazimia kuwa chama hicho kitaendelea kuelimisha na kuhamasisha Watanzania umuhimu wa kuwa na katiba mpya yenye kukidhi mfumo wa vyama vingi vya siasa.
“Tutafanya kwa njia mbalimba ikiwemo maridhiano ya kitaifa yenye misingi ya maelewano, maendeleo, umoja na amani katika makundi yote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Mbatia.
Aidha alisema Halmashari Kuu imeazimia kwamba kwa kuwa Tanzania ni sehemu ya dunia na lengo la 17 la Malengo Endelevu ya Dunia ni ushirikiano wenye masilahi kwa pande zote, wanatoa rai kwa Watanzania wote kushirikiana kwa utulivu.
“Tunatoa rai kwa Watanzania wote wenye nia njema ya maendeleo endelevu ya nchi yetu tusikilizane, tushikamande na kushirikiana tukiwa watulivu kuhakikisha nchi yetu inaendela kuwa ya mfumo wa vyama vingi vya siasa,”alisema Mwenyekiti huyo wa NCCR Mageuzi.